Solskjaer atoa kauli kuhusu usajili wa beki wa kati Man Utd

MANCHESTER, ENGLAND. MMEELEWA? Manchester United hataingia sokoni kufanya usajili wa beki yeyote wa kati kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ambalo limebaki wiki moja tu kufungwa rasmi.

Hiyo ni kwa mujibu wa kocha wa miamba hiyo ya Old Trafford, Ole Gunnar Solskjaer kwamba, haoni kama kikosi chake kina shida ya kufanya usajili wa beki wa kati kwa sasa.

Kocha huyo raia wa Norway, kwa msisitizo alisema kikosi chake kina mabeki wa wazuri sana, tatizo lililopo kwa sasa ni kwamba wanahitaji kunolewa tu ili kurudi kwenye makali yao. Safu ya mabeki ya Man United ilikosolewa vikali kwenye mchezo wa Brighton kutokana na aina ya mabao iliyoruhusu kwenye ushindi wa 3-2, huku ukuta huo ulifanya makosa ya kizembe kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England walipochapwa 3-1 na Crystal Palace uwanjani Old Trafford.

Viwango vya mabeki wa timu hiyo katika mechi hizo mbili vilizua mjadala na wachambuzi wa mambo ya soka kumpa tahadhari Solskjaer kwamba, anahitaji kufanya usajili wa beki wa kati wa kiwango cha dunia ili kwenda kucheza pamoja na Harry Maguire baada ya Victor Lindelof kuonekana kuwa ni majanga makubwa.

Hata hivyo, hadi sasa wakati dirisha la usajili likiwa limebakiza siku chache kufungwa, Man United imesajili mchezaji mmoja tu, kiungo wa Kidachi Donny van de Beek iliyomnasa kutoka Ajax kwa ada ya uhamisho ya Pauni 39 milioni.

Na Solskjaer wala hana mpango wa kusajili beki licha ya kutakiwa kufanya hivyo kutokana na makosa mengi yaliyoonyeshwa na safu ya ulinzi ya timu hiyo kwenye mechi mbili zilizopita, tena ikicheza dhidi ya timu za kawaida tu.

Solskjaer alisema: “Tuna mabeki wengi sana na nilimwingiza Eric (Bailly) kusaidia kwenye kukaba kutokana na mikimbio ya (Leandro) Trossard na (Neal) Maupay.

“Kwa upande wangu, naona tuna mabeki wengi wa kati wapo kwenye timu yetu kwa sasa. Unaporuhusu nafasi na kuruhusu mabao, kuna mambo mawili tofauti kabisa unayoweza kuyafanyia kazi - ama timu haina makali au kuna makosa binafsi yanafanyika uwanjani.

“Kama timu hatupo kwenye ubora wetu, hatupo kwenye kiwango chetu, hatuna ubora wa kutosha wa kuzuia krosi zisipigwe au kuwakimbiza wanaokimbilia golini kwetu.

Tulikuwa nyuma kwa kiasi fulani, hayo ni makosa mjumuiko na si ya mtu mmoja mmoja. Nadhani Victor (Lindelof) alifanya vizuri.”

Wakati Solskjaer akiamini safu yake ya mabeki, wapo wanaoamini kwamba shida ya ubovu wa beki ya miamba hiyo inaanzia kwenye kiungo.

Kiungo wa zamani wa Liverpool, Danny Murphy alisema: “Manchester United itaendelea kufungwa mabao kama itaendelea kuwapanga Paul Pogba na Bruno Fernandes kwa pamoja.

“Ni wachezaji wazuri sana wabunifu, lakini hakuna hata mmoja mwenye uwezo wa kukaba unapowachezesha pamoja kwenye safu ya viungo watatu. Hilo litakuwa tatizo kubwa sana watakapocheza dhidi ya timu za Big Six kwa sababu kilichotokea Jumamosi dhidi ya Brighton ni uthibitisho tu.

“Udhaifu wao wa kushindwa kukaba unawaweka mabeki wa pembeni Aaron Wan-Bissaka na Luke Shaw kwenye matatizo makubwa kwa sababu walikuwa wakiandamwa moja kwa moja na washambuliaji wa pembeni wa Brighton. Ni lazima Ole atafute suluhisho.”