Solskjaer amchimba mkwara Mino Raiola

Muktasari:

Wikiendi iliyopita, Raiola amemzungumzia kiungo Pogba akidai nafasi za chini inayoshika Man Unnited kwenye ligi haiendani kabisa na matakwa ya mchezaji huyo.

MANCHESTER, ENGLAND . VITA imekolea. Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemwambia wakala Mino Raiola: “Mimi ndiye nitakayeamua nini kitokee kwa Paul Pogba -sio wewe.”

Wakala Raiola amewachimba mkwara tena Man United juu ya mchezaji wao huyo waliyemsajili kwa Pauni 89 milioni kwamba, ataondoka na kuachana na timu hiyo kama watashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Lakini kiungo Pogba bado ana mkataba wa miezi 16 katika kikosi hicho cha Old Trafford, ambapo ndani yake kuna kipengele cha Man United kumwongezea mwaka mmoja wanapoona inabidi.

Hata hivyo, Man United wanafikiria kumuuza kwa Pauni 150 milioni, lakini hilo kama wataamua wenyewe na si kupangiwa na mtu.

Solskjaer alisema: “Paul ni mchezaji wetu sio mchezaji wa Mino.

“Sijawahi kukaa chini kumwambia Pogba kitu gani anapaswa kumwambia wakala wake aseme na kitu gani asiseme.”

Wikiendi iliyopita, Raiola amemzungumzia kiungo Pogba akidai nafasi za chini inayoshika Man Unnited kwenye ligi haiendani kabisa na matakwa ya mchezaji huyo.

Raiola alisema: “Paul anataka kubaki kwenye viwango vya juu. Tusubiri kuona mwisho wa msimu itakavyokuwa kama atabaki au la.”

Kwenye hilo, wakala Raiola alisema kuna uwezekano mkubwa wa staa huyo akarudi zake Juventus.