Solskjaer abatizwa kwa moto, PSG yaichapa Man United

Muktasari:

 

  • Paris Saint-Germain inakuwa timu ya kwanza kutoka Ufaransa kuifunga Manchester United kwenye Uwanja Old Trafford katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

London, England. Manchester United inahitaji muujiza mkubwa kufufua matumaini yake katika Ligi ya Mabingwa baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Paris St-Germain kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Hakuna timu kati 34 zinazoshiriki mashindano hayo ambayo katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ilifungwa nyumbani mabao mawili au zaidi ikafanikiwa kusonga mbele.

Mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Presnel Kimpembe na Kylian Mbappe umewapa ushindi mnono mabingwa wa Ufaransa, huku Paul Pogba akitolewa nje kwa kadi mbili za njano.

Man United iliyokuwa imeshinda mechi 10 kati ya 11 chini ya kocha wa muda Ole Gunnar Solskjaer ilikuwa na matumaini ya kuendeleza mafanikio hayo katika mashindano hayo makubwa Ulaya.

Badala yake, Man United ikapotezwa na PSG na kupokea kipigo cha kwanza nyumbani cha zaidi ya bao moja na sasa wanatakiwa kufanya kazi ya ziada jijini Paris hapo Machi 6, ili kusonga mbele kwa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Matumaini ya Solskjaer yalianza vibaya katika kipindi cha kwanza kwa kupata majeruhi Jesse Lingard na Anthony Martial, lakini PSG haikuonyesha tofauti yoyote pamoja na kukosekana kwa nyota wake wawili Neymar na Edinson Cavani.

Nyota wa zamani wa Manchester United, Angel Di Maria aliyekuwa nyota wa mchezo alisababisha bao la kwanza dakika 53, kwa mpira wake wa kona kumaliziwa na Kimpembe, aliyeweza kumtoka Nemanja Matic na kupiga shuti lililompita David De Gea.

Mshambuliaji Mbappe akiwa katika kiwango bora alitumia vizuri pasi ya Di Maria kufunga bao la pili kwa PSG.

Usiku huo mbaya kwa United ulitimishwa kwa kiungo wake Pogba kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano katika dakika za mwishoni hivyo atakosa mechi ya marudiano.

Solskjaer amefanya kazi nzuri ya kurudisha Man United katika ubora wake tangu alipochukua mikoba ya Jose Mourinho mwezi Desemba mwaka jana – lakini alikuwa na usiku mgumu zaidi tangu alipotua Old Trafford.

Haikuonyesha kuwa sababu ni Solskjaer ndiyo kimechangia kipigo cha Man United, ila ni madhara ya kukutana na timu bora ikiwa na washambuliaji mahiri Di Maria na Mbappe, pamoja na kukosekana kwa Neymar na Cavani.

Solskjaer na Man United kwa upande wao hawakupata msaada wa majeruhi ya Lingard na Martial mwanzoni mwa mchezo huo.

Man United haikupoteza kwa sababu ya uwezo au kiwango chao, lakini walikosa silaha za kuivunja ngome ya Thomas Tuchel kama PSG ilikuwa ikifanya kwa ngome ya Man United kupitia kwa Di Maria pamoja Mbappe.

Solskjaer hajakata tamaa kuelekea katika mchezo wa marudiano jijini Paris, lakini mazingira yanaonyesha kama ndiyo mwisho wa safari ya Manchester United katika Ligi ya Mabingwa.