Solskjaer aambiwa ushindi dhidi ya Spurs bado haumsaidii

Muktasari:

Baada ya matokeo ya hovyo mfululizo jambo hilo lilimfanya Solskjaer kuwa kwenye presha kubwa ya kupoteza ajira yake huku kocha wa zamani wa Spurs, Mauricio Pochettino akihusishwa na miamba hiyo ya Old Trafford na kama angepoteza dhidi ya Spurs basi hali ingekuwa mbaya zaidi kwa upande wake.

MANCHESTER, ENGLAND. KIPA wa zamani wa Manchester United, Peter Schmeichel amesema haisaidii kitu na kwamba kocha Ole Gunnar Solskjaer ataendelea kuwa na presha juu ya usalama wa kibarua chake hata kama timu yake imecheza vizuri na kushinda 2-1 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England juzi Jumatano.

Mabao mawili ya Marcus Rashford yaliisaidia Man United kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo wakimwaadhibu kocha wao wa zamani, Jose Mourinho, ambaye kwa sasa anainoa Spurs.

Baada ya matokeo ya hovyo mfululizo jambo hilo lilimfanya Solskjaer kuwa kwenye presha kubwa ya kupoteza ajira yake huku kocha wa zamani wa Spurs, Mauricio Pochettino akihusishwa na miamba hiyo ya Old Trafford na kama angepoteza dhidi ya Spurs basi hali ingekuwa mbaya zaidi kwa upande wake.

Hata hivyo, Schmeichel anaamini kwamba matokeo ya juzi hayawezi kumweka salama Solskjaer, akisema: "Matokeo yatampa amani ya siku chache tu, lakini furaha yake itaisha kwenye mechi ijayo akipoteza. Ana timu changa sana na tusisahau kwamba amekuwa kwenye hali mbaya kwenye timu hiyo.

"Yupo kwenye presha kubwa. Yupo kwenye orodha ya kocha anayefuatia kufutwa kazi. Pengine anaweza kuwa (Marco) Silva huko Everton kwamba akamtangulia kufukuzwa."

Schmeichel amekiri kwamba alikuwa kwenye wasiwasi mkubwa akitazama Man United ikicheza na timu inayonolewa nan Mourinho, lakini alisema alivutiwa na kiwango cha timu yake ya zamani hasa baada ya kutuliza akili yao na kusaka ushindi kufuatia bao la kusawazisha na Dele Alli, kwamba halikuwavuruga. Ushindi huo uliwaondoa Man United kwenye nafasi ya 10 na kupanda juu kidogo, lakini Jumamosi watakuwa na shughuli pevu kwa kuwakabili Manchester City uwanjani Etihad.