Soka limempa mke Massawe

Muktasari:

  • Mwanaspoti lilimnasa na kupiga naye stori, amefunguka mambo mengi ya ndani na nje ya uwanjani, ikiwemo na alivyofanyiwa ushirikina akiwa Ndanda FC, kilichomuokoa ni kumpa ukweli mhusika ambaye ni rafiki yake mkubwa mpaka sasa.

JACOB Massawe ukipenda muite ‘Le Captain’ ni miongoni mwa wachezaji wazawa ambao wanafanya vitu vikubwa, amechezea timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara (TPL), ameacha alama ya mchango wake na sasa ana kasi ya kuzifumania nyavu, kubwa zaidi anaweza akacheza namba zote ndani kasoro kipa.

Ametoka mbali mpaka kufikia hatua ya kujulikana nchini, juhudi, nidhamu na kupenda kujifunza kila siku, vimemchangia kwa asilimia kubwa kufika alipo kwa sasa isipokuwa kitu anachokitamani zaidi ni kulitumikia taifa lake kupitia Taifa Stars.

Mwanaspoti lilimnasa na kupiga naye stori, amefunguka mambo mengi ya ndani na nje ya uwanjani, ikiwemo na alivyofanyiwa ushirikina akiwa Ndanda FC, kilichomuokoa ni kumpa ukweli mhusika ambaye ni rafiki yake mkubwa mpaka sasa.

ANACHEZA NAFASI TOFAUTI

Massawe anasema akiwa Ndanda, alikuwa anachezeshwa kama beki namba mbili na Kocha Hamsini Malale na anakiri aliweza kumudu namba hiyo vyema, “Nilicheza kwa mafanikio makubwa ingawa mechi ya za mwisho wakati timu inataka kushuka nikawa nacheza winga,” anasema.

Akiwa na Toto African alikuwa anacheza kama kiungo wa chini akiwa chini ya kocha John Tegete, lakini baada ya kujiunga na African Lyon alibadilishwa na kucheza kama kiungo, kali zaidi akiwa Mwadui FC alikuwa anachezeshwa kama kiungo mkabaji.

“Kila kocha amenipanga namba yake, lakini nilimudu na kucheza vyema, hiki ndicho kitu ninachoweza kumshukuru Mungu, isipokuwa sijawahi kuchezeshwa kipa,” anasema.

TOTO ILIMPA UJASIRI

Toto Africans ndio timu yake ya kwanza kuichezea Ligi Kuu Bara, dau lake la usajili lilikuwa Shi1.5 ambazo anaeleza kwamba alizitumia kununua vyombo vya ndani vya kuanzia maisha na anakiri ndio ilikuwa pesa yake kubwa kuikamata mkononi.

Ulikuwa msimu wa 2011/12 ambao kwake ulikuwa mzuri, akifichua kwamba alicheza mechi bila kufanyiwa mabadiliko, kipindi hicho zilikuwa zinashiriki timu 14 ambapo alitumia dakika 1,260.

“Ni msimu ambao natamani ujirudie maishani mwangu kwani nilikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu ambacho timu nyingi zilinitolea macho,”anasema.

Msimu huo Toto ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya 11 na pointi 26 huku Villa Squad, Moro United na Polisi Dodoma zikishuka daraja na kuzipisha Mgambo JKT, Tanzania Prisons na Polisi Morogoro zikipanda kucheza Ligi Kuu.

TUZO YAMPA MKE

Akiwa Toto Africans msimu wake wa kwanza 2010/11 alifanikiwa kuibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara, alikabidhiwa zawadi ya Sh2,650,000 ambazo alienda kutoa mali ya kumuoa mke wake Beatrice anayeishi naye na wamefanikiwa kupata mtoto mmoja.

Anasema tukio hilo ni kubwa kwake ambalo hatakaa alisahau katika maisha yake ya soka, ingawa kwa sasa amekiri kufanikiwa zaidi kuliko alikotoka ambako anakuita mwanzo mgumu.

“Mtu akiniuliza soka limenilipa, jambo la kwanza bila kusita sita nitamjibu ndio kwani nisingepata pesa ya zawadi, nadhani isingekuwa rahisi kupata pesa za kutoa maali ya kuoa.

“Wanaume tupo hivi, ukitokea ukamuelewa mwanamke wa kuishi naye, halafu ukawa hauna kitu mkononi huo ni mtihani mkubwa kwako, nilikuwa nawaza na ilinisaidia kujituma kwa bidii mpaka nikawa mchezaji bora nikafanikisha ndoto zangu,” anasema.

ATUA AFRICAN LYON

Msimu wa 2012/13 alisajiliwa na African Lyon, huku akiwa na matumaini makubwa ya kufika mbali, lakini mambo yakamwendea kombo na kujikuta akiangukia Mwadui FC iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

“Mwadui FC nilicheza mwaka mmoja kisha nikaenda kujiunga na JKT Oljoro ikiwa Ligi Kuu, huku sikuwa kuwa nahodha, pia sikuwa na mafanikio makubwa sana.

“Baadaye nikaenda kujiunga Ndanda ambayo nilicheza kwa mafanikio na nilimaliza msimu nikiwa na mabao saba,” anasema.

HISTORIA YAKE NA STAND

Anasema akiwa na Lyon, muda wa likizo alikuwa akirudi mkoani kwao Shinyanga, ambako alikuwa anafanya mazoezi na Medical FC ambayo kwa sasa ni Stand United ‘Chama la Wana’ yeye akiwa miongoni mwa waliochangia kufika ilipo.

Masawe anasema kulitokea mashindano ya RPC ambapo yeye alikuwa mfungaji bora kwa mabao saba na timu hiyo ndio iliibuka mabingwa anafichua hapo ndipo walipopata wazo la kubadili jina kutoka Medical FC na kuitwa Stand United ‘Chama la Wana.

“Baada ya kuona timu ina wachezaji ambao wanajituma waliokuwa wanafanya kazi standi, baadhi walikuwa waendesha bodaboda na wengine wapiga debe, tukasema haitakuwa mbaya kama timu itaitwa Stand United ‘Chama la Wana’.

“Tulikuwepo wachezaji wengi baadhi yao ni Paul Nonga, Idd Mobby na wengine wengi, tukaendakumwambia mbunge wa mkoa huu Steven Masele akalipitisha na akaunga mkono juhudi hizo mpaka leo anasaidia sana kuhakikisha inafika mbali hasa baada ya kupanda Ligi Kuu timu hiyo.

Je, unajua ndani ya Stand United kulitokea mpasuko mkubwa, huku Massawe akionekana ndio chanzo? Usikose kufuatilia undani wa hilo kesho Ijumaa ndani ya Mwanaspoti.