Sofapaka wameanza kushika Rada

Muktasari:

Mabingwa hao wa Ligi Kuu 2009 watafungua msimu mpya kwa kukwaruzana na Posta Rangers walioponea kushushwa daraja msimu uliopita kwa tundu la sindano.

KOCHA mpya wa Sofapaka Divaldop Alves kasema vijana wake wameanza kushika rada yake tangu alipochukua majukumu ya kuwafunza wiki iliyopita.

Kauli yake Alves imetoka baada ya vijana wake kutoka sare ya 1-1 na Ushuru FC  ya divisheni ya pili, kwenye mechi ya kirafiki wikendi iliyopita.

Kwenye harakati zake za kutesti mitambo, Kocha Alves alihakikisha amewachezesha wachezaji wote aliokuwa nao ili kuweza kupata picha kamili ya uwezo wao.

“Tangu nije, wachezaji wamezidi kuimarisha viwango vyao, wameanza kunielewa. Katika kipindi cha kwanza tulifurahia kuona uzalishaji wa krosi za kutosha. Ni mbinu ambayo tumekuwa tukifanya kazi mazoezini na kuona ule utandaji, ni jambo la kufurahisha sana,” Alves alielezea.

Kulingana naye, anasema staili yake itakuwa ya kushambulia zaidi na ndio maana mbinu ya uzalishaji krosi kutoka kwa wachezaji wa pembeni ni la kimsingi sana kwenye filosofia yake ya ukocha.

“Bado hatujaiva sababu tunahitaji sana kuzidisha ubora wetu kwenye mbinu zetu za ushambuliaji,” Alves kaongeza.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu 2009 watafungua msimu mpya kwa kukwaruzana na Posta Rangers walioponea kushushwa daraja msimu uliopita kwa tundu la sindano.