Skendo ya hirizi yamkera Chege

KWA mashabiki wa muziki wa kizazi kipya na hasa wale wa TMK Wanaume Family, wanaijua kazi nzito ya Chege Chigunda.

Mwimbaji huyo aliyeanza kufahamika kupitia kundi la Manyema Family, ni mmoja kati ya wasanii walioipaisha TMK na kujenga jeshi la maangamizi akishirikiana na Mhe. Temba na wakali wengine wa kundi hilo lililotikisa vilivyo nchini.

Kama umeshawahi kuzisikia nyimbo matata za Dar Mpaka Moro, Wanaume Kazini, Ndio Zetu, Umri Unakwenda na nyingine ni kati ya kazi za Chege na wenzake. Pia mbali na nyimbo za kundi, mkali huyo ameachia kazi mbalimbali kama, Mkono Mmoja, Sweety Sweety, Go Down, Waache Waoane, Run Town, Wafoo na Kaitaba.

Majina halisi ya staa huyu ni Saidi Juma Hassan ‘Chege Chigunda’ a.k.a Mtoto wa Mama Said. Mwanaspoti limefanya mahojiano naye na jamaa kufunga mengi. Hebu tiririka naye upate uhondo kamili...!

Mwanaspoti: Mambo vipi?

Chege: Poa, niambie,

Mwanaspoti: Kitu gani usichokipenda katika maisha yako?

Chege: Nawachukia sana wanaopenda kukwamisha maendeleo yangu na wezi wa kazi zetu kwa jumla.

Mwanaspoti: Mpangilio mzima na ratiba yako kwa siku umekaaje?

Chege: Mara nyingi ninapokuwa bize na mazoezi ya wimbo mpya, huwa naamka saa nne asubuhi. Ninaporudi home nahitaji muda mwingi wa kukaa na kuandika nyimbo mpya nyingine, baadae najipumzisha.

Mwanaspoti: Hongera kwa kupata mtoto wa kike, maana hatujawasiliana tangu upate mtoto, lakini kuna madai kuwa umezaa na mwanamke wa mtu ni kweli?

Chege: Asante kwa hongera zako, ila hayo madai unayosema ni ya miaka sita iliyopita, kuna dada anayeitwa Salma, kuna jamaa alisema ni mwanamke wake, ila watu wasichanganye mafaili bwana. Huyu niliyezaa naye ni Zahra ni mwanamke wangu wa siku nyingi sana tumepata mtoto miezi michache iliyopita.

Mwanaspoti: Kwenye suala zima la kujiachia, yaani kwenda katika sehemu mbalimbali za starehe kwako limekaaje?

Chege: Hilo lipo, siku moja moja natoka na rafiki zangu wa kitaa wananipitia tunaenda kujichanganya maeneo tofauti. Si unajua kazi na dawa wakati mwingine.

Mwanaspoti: Huwa unapenda kuandika mashairi wakati gani, ikiwemo kuingiza sauti studio?

Chege: Mara nyingi hutegemea na mazingira, naandika wakati wowote, kuhusu kuingiza sauti (kurekodi) huwa inategemea na ratiba za studio.

Mwanaspoti: Ni skendo gani hutaisahau maishani mwako toka umepata umaarufu?

Chege: Daah! Asikwambie mtu skendo ya kuambiwa mshirikina yaani natumia ndumba nikipanda stejini.

Mwanaspoti: Ilikuwaje hadi ukaambiwa hivyo?

Chege: Kuna picha iliwekwa mtandaoni ikinionyesha nimenyoosha mkono mmoja juu na kuonekana nimevaa kitambaa cheusi nimekifunga karibu na bega, basi watu wakaanza kusema ni hirizi.

Kiukweli nilikerwa sana na sitaweza kusahau, mimi nilivaa kitambaa hicho cheusi ili kumuenzi mwanamuziki Mez B aliyekuwa amefariki kipindi hicho.Tena hiyo ilikuwa katika bonanza lililopigwa Dodoma la PSPF mwaka 2015

Mwanaspoti: Hivi sasa ukipata tatizo mtu gani wa kwanza kumkimbilia?

Chege: Wa kwanza ni mama yangu mzazi kwa kuwa ndiye yuko karibu sana na mimi.

Mwanaspoti: Unapendelea msosi wa aina gani?

Chege: Kwenye suala la misosi huwa sichagui, wowote unaokubali kuingia kinywani huwa nakandamiza tu.

Mwanaspoti: Poa Chege, pamoja sana.

Chege: Nashukuru, karibu tena.