Siyo janga kufungwa na Sevilla, Simba imetisha

Muktasari:

Sevilla ni klabu ya hadhi ya juu sana. Waulize Barcelona, waulize Real Madrid, waulize Manchester United. Kwa nyakati tofauti miamba hao wa soka Ulaya na wengine wengi wameshakumbana na moto wa Sevilla.

TUNAPOZUNGUMZIA matumaini ya kuanza kukua kwa soka la Tanzania, tunamaanisha matokeo kama yale waliyopata Simba dhidi ya Sevilla kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.

Ndiyo Simba ilifungwa 5-4. Ndiyo Simba Sevilla walikuwa wakicheza kama mazoezi. Ndiyo nyota wa Sevilla hawakuwa na chochote wanachokitafuta katika mechi ile mbali na kujaribu tu kuepuka majeraha maana kipindi cha usajili kimeshaanza na miguu yao ina thamani ya mamilioni ya Euro.

Lakini bado kwa ‘levo’ zao, na ‘levo’ zetu, hata kama nyota wale hawakuwa na wanachokipigania, kwa matokeo waliyoyapata Simba ni jambo la kujivunia sana.

Kufunga magoli manne dhidi ya mabingwa mara nne wa Europa, matatu ndani ya dakika 30 hata kama ni mazoezini si jambo la kupuuzwa.

Sevilla ni klabu ya hadhi ya juu sana. Waulize Barcelona, waulize Real Madrid, waulize Manchester United. Kwa nyakati tofauti miamba hao wa soka Ulaya na wengine wengi wameshakumbana na moto wa Sevilla.

Ni klabu inayotisha katika Ligi Kuu ya Hispania na Ulaya kwa ujumla.

Si timu ambayo utaomba kukutana nayo katika mechi yoyote iwe ligi ama mtoano.

Ni msimu huu huu, Sevilla waliisambaratisha Real Madrid kwa kipigo cha 3-0 kwenye Uwanja wa Ramon Sanchez Pizjuan kupitia magoli mawili ya Andre Silva na Wissam Ben Yedder. katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Hispania huku winga Jesus Navas akimtia njaa balaa beki wa kushoto wa Kibrazil, Marcelo.

Kiufupi Sevilla ni timu kubwa ambayo haihitaji ufafanuzi katika kuielezea. Kutaja jina lake tu linatosha kumfanya shabiki yeyote anayejua mpira kuwapigia saluti.

Ndiyo maana tunasema kitendo cha Simba kwenda nao uso kwa uso na kuongoza 2-0, kisha 3-1 na kisha 4-2, ni jambao linalotosha kuwafanya waende vifua mbele wakitambua kwamba kuna kitu kimeanza kutengeezwa katika soka la Bongo.

Kitendo cha straika na nahodha wa Simba, John Bocco kushinda tuzo ya Nyota wa Mchezo huo baada ya kufunga magoli mawili na kutoa ‘asisti’ moja ni jambo linalotosha kuinua macho ya wageni kupenda kumfahamu vizuri mchezaji huyo. Bahati mbaya tu kwa Bocco ni kwamba umri unamsaliti. Miezi mitatu ijayo anatimiza wa miaka 30 ya kuzaliwa ya ‘pasipoti’. Hawezi kuwavuta mawakala kuja kumuangalia kwa mara ya pili.

Lakini Simba ilipiga mpira unaoeleweka na ilifika wakati ilionekana ingeweza kushinda magoli mengi zaidi.

Magoli mazuri kutoka kwa Bocco, Meddie Kagere na Clatous Chama, yalionekana kuwavuruga hata Sevilla wenyewe ambao walikuwa wakicheza kwa kujiachia mno na walionekana wazi hawakutarajia kama Simba ingeweza kupata magoli yote yale mbele yao hata kama wanacheza kwa kudharau kiasi gani.

Kung’aa mbele ya mastaa wa kiwango cha dunia kama Jesus Navas, Ever Banega, Ben Yedder, Nolito, Aleix Vidal aliyetokea Barcelona, siyo jambo dogo.

Licha ya kupoteza mechi ile ya kirafiki juzi, Simba ina mengi ya kujivunia katika mechi ile na msimu mzima kwa ujumla.

Huu umekuwa msimu wa mafanikio makubwa kwa Simba baada ya kukinukisha katika Ligi ya Mabingwa Afrika hadi hatua ya robo-fainali walikotolewa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Ni msimu wa kujivunia kupambana hadi kubeba taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa msimu wa pili mfululizo.

Kila kitu kina mwanzo na Simba imeonyesha matumaini makubwa katika safari yake hiyo mpya.

Ndiyo kwanza imeanza kuendeshwa kufuata mfumo mpya wa uwekezaji chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed ‘Mo’ Dewji kutoka katika mfumo uliolidumaza soka la Tanzania kwa miaka mingi la wanachama.

Hivyo, mafanikio yoyote wanayoyapata Simba sasa, yanapaswa kutumiwa na klabu nyingine za Tanzania kama somo katika kutafuta mifumo bora ya kisasa inayopaswa kufuatwa katika kuendesha klabu zao na kuinua viwango vyao kiuchumi na kiushindani.

Kwa waliyoyafanya mwaka huu Simba, unaweza kujiuliza ni nani ataweza kuwazuia Wekundu wa Msimbazi wasiendelee kutawala soka la Bongo kwa miaka ya karibuni?

Kama vIlabu vingine havitabadilisha staili zilizotumia msimu huu, Wekundu wa Msimbazi watabaki kuwa juu juu ambapo wapo baada ya kufanya mengi yatakayobaki katika vitabu vya historia ya soka la Bongo.