Siro, baba wa Mo wazungumza

Muktasari:

  • Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji 'Mo Dewji'. Bilionea huyo alitekwa Alhamisi asubuhi Oktoba 11, 2018 katiika hoteli ya Colossium jijini Dar es Salaam alikokwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Siro aliliambia Mwanspoti jana kuwa, polisi bado wanaendelea na upelelezi wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji, huku akiahidi kutoa taarifa zaidi leo.

Sirro aliyasema hayo alipokuwa kwenye maziko ya aliyekuwa mhasibu wa jeshi hilo, Arcado Nchinga yaliyofanyika katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Hapa niko msibani siwezi kuzungumza lolote, mambo ya upelelezi yana mahala pake. Naomba mnipe nafasi hadi kesho asubuhi,” alisema Sirro.

Kwa upande wake, baba wa mfanyabiashara huyo, Gulam Dewji Hussein alipotafutwa na Mwanspoti kuzungumzia taarifa zozote kuhusu mwanaye, alisema familia ilikuwa haijapata chochote kutoka polisi hadi jana jioni.

Alipoulizwa kuhusu simu ya mwanaye inayosemekana ikipigwa inaita na kupokea ujumbe mfupi wa maandishi (sms), mzazi huyo alimtaka mwandishi wa habari hizi asubiri kwa kuwa muda huo (wa jioni) alikuwa na wageni na asingeweza kuzungumzia suala hilo. Hata alipotafutwa baadaye hakuweza kupatikana.