Siri yafichuka, vipigo vya Alliance

Muktasari:

  • Malale ambaye alitokea Ndanda tayari ameiongoza Alliance FC katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar ilipolala kwa bao 1-0 pamoja na Mwadui FC ambayo ilicharazwa mabao 4-0.

KOCHA Mkuu wa Alliance FC, Malale Hamsini hajapata ushindi wowote kwenye mechi zake mbili alizosimamia hadi sasa lakini ameibuka na kutaja sababu nne zilizowagharimu kwa kupata matokeo hayo yasiyoridhisha.

Malale ambaye alitokea Ndanda tayari ameiongoza Alliance FC katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar ilipolala kwa bao 1-0 pamoja na Mwadui FC ambayo ilicharazwa mabao 4-0.

Kutokana na matokeo hayo, Malale alisema uchoyo, kutokuwa na maamuzi ya kupiga mashuti golini, kutotofautisha mechi za nyumbani na ugenini na kupiga chenga nyingi ndizo sababu zilizoigharimu timu katika mechi hizo.

Alisema kwa sasa ndio anaiandaa rasmi timu kuhakikisha wachezaji wanaachana na kucheza mpira waliouzoea badala yake wabadilike, kwani anachotaka ni ushindi tu.

“Sababu zipo nne, kwanza hawajatofautisha mechi za nyumbani na ugenini kucheza kiushindani, kupiga chenga nyingi, kutokuwa na maamuzi wakiwa eneo la hatari na uchoyo, ila watabadilika,” alisisitiza Hamsini.

Aliongeza bado hajavutiwa na kasi ya washambuliaji wake kutokana na kuwa na mabao machache tofauti wachezaji wa timu nyingine.

Alisema licha ya wachezaji kucheza vizuri lakini bado ana kazi ngumu ya kusaka ushindi.

“Bado washambuliaji wangu hawajaonyesha uwezo, mtu ana mabao mawili eti ni straika? Lazima wabadilike kama wachezaji kwahiyo bado nina kazi ya kutafuta matokeo ili kukaa nafasi nzuri.”