Siri ya Ngassa kubaki Yanga yafichuka

Muktasari:

Anaendelea kusema udanganyifu wa wachezaji wengi unawafanya thamani yao ipungue kwa viongozi hasa Simba na Yanga, akisisitiza kwamba bora wanapozihama klabu hizo wawe wawazi ili kuwapa muda kamati za usajili kutafuta mbadala wao.

STAA wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amefichua siri ya Mrisho Ngassa kupewa nafasi katika timu hiyo, kwamba ni uzalendo aliouonyesha wakati anaondoka kwenda Afrika Kusini klabu ya Free State.
Lunyamila anasema Ngassa aliondoka kwa amani  ndani ya Yanga, jambo analoamini limemrahisishia kufikiriwa kwa wepesi na viongozi wa klabu hiyo.
Amefafanua kwa nini amemtolea mfano Ngassa, akitaja sababu za wachezaji wanaohama Simba na Yanga kama vita akitaka wajifunze kwamba maisha ya mpira ni amani hivyo wanapaswa kuwa wawazi ili siku wakirejea wasipate shida.
Anaendelea kusema udanganyifu wa wachezaji wengi unawafanya thamani yao ipungue kwa viongozi hasa Simba na Yanga, akisisitiza kwamba bora wanapozihama klabu hizo wawe wawazi ili kuwapa muda kamati za usajili kutafuta mbadala wao.
"Kama umefanya kazi vizuri na kwa amani basi unaaga tu vizuri, kwani soka ni kazi yao inatakiwa kwao popote iwe kambi, lakini tabia ya kuwapotezea watu muda kukufuatilia mtu ambaye huna malengo ya kuendelea kuwepo hapo sio nzuri na inaleta chuki.
" Mfano Ngassa sidhani kama angekuwa na nafasi Yanga kama asingeaga kwa amani, hilo liliwasaidia viongozi wa kipindi hicho kutafuta mbadala wake mapema, hata Simba ndio maana Emmanuel Okwi amekuwa anaondoka na kurejea na anapokelewa vizuri," anasema.