Sir Alex Ferguson awapa tano Liverpool

Saturday June 27 2020
fergie pic

London, England. Kocha na mchezaji wa  zamani wa Liverpool, Kenny Dalglish amefichua kuwa kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson  amewatumia ujumbe wa pongezi baada ya Liverpool  kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) juzi Alhamisi.

Ushindi wa mabao  2-1 ambao waliupata Chelsea  dhidi ya Manchester City uliifanya Liverpool itangazwe rasmi kuwa bingwa wa taji hilo msimu huu huku wakiwa na  michezo saba mbele yao kabla ya msimu kumalizika.

Liverpool wanaongoza msimamo kwa tofauti ya pointi 23 ambazo hakuna klabu inayoweza kuzifikia.

Lakini licha ya  uhasama mkali uliopo baina ya Liverpool na United, Ferguson aliweka kando  hilo na kutoa pongezi ambazo  Dalglish amekoshwa nazo.

"Amewasiliana nasi kusema hongereni - haupo vitani!" Dalglish alinukuliwa akisema.

"Kuna ushindani kati ya maadui wote wa zamani, lakini mwishoni mwa mwaka unapeleka ujumbe wa  pongezi kusema umefanya vizuri.

Advertisement

"Hiyo inaendelea na ni pongezi nzuri. Unaweza kuwa mpinzani lakini unapaswa kuwa na ujasiri wa kutuma ujumbe wa pongezi.

"Watu ambao umekuwa ukishindana na maisha yako yote katika mpira wa miguu, wangetamani ni wao wenyewe walioshinda, lakini wanajivunia kuwaheshimu watu wengine pia,” alisema Dalglish

 Makocha hao wawili wa zamani, walikuwa na tabia za kutupiana maneno wakati wakishindana katika mikiki ya Ligi Kuu  ya England

Advertisement