Sio Etienne, Yanga kuna watatu

Thursday August 13 2020

 

By Mwandishi Wetu

YANGA wameshafanya mazungumzo ya awali na Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije na inaelezwa pia ndiye amehusika kwenye sehemu kubwa ya usajili unaoendelea klabuni hapo.

Lakini tetesi zinadai pia baadhi ya vigogo wanashawishi achukuliwe kocha mmoja kutoka Ufaransa ambaye wasifu wake ni mkubwa kuliko ule wa Etienne.

Habari za ndani zinasema kwamba bado mzozo upo baina yao, ingawa kuna wengine wanasema achukuliwe Etienne tu kwa vile ana uzoefu na soka la Tanzania na amepata mafanikio makubwa kama ilivyokuwa kwa Patrick Aussems ambaye amependekezwa pia na wajumbe wachache kutokana na mafanikio aliyopata ndani ya Simba.

Inaelezwa kwamba kabla ya mwisho wa wiki hii Yanga itakuwa imeshaamua jina moja kati ya Mfaransa huyo au Etienne.

Kocha Etienne ana uzoefu wa soka la Tanzania kwani alianza kuinoa Mbao ilipopanda Ligi Kuu mwaka 2016, kisha akatua KMC na baadaye kunyakuliwa na Azam kabla ya kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa Stars. Akiwa Stars, Etienne aliiwezesha kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) kwa kuzing’oa Kenya, Burundi na Sudan kwenye mechi za mchujo.

Advertisement