Singida United yazidi kutajirika

Tuesday July 4 2017

By THOBIAS SEBASTIAN

SINGIDA United jana Jumatatu ilitambulisha basi la timu ambalo watalitumia msimu ujao lenye thamani ya Sh350 milioni. Mkurugenzi wa Singida United, Richard Festo alisema wana wadhamini saba ambapo watano kati yao wameshawapa mkwanja.

Lakini siku si nyingi watawatangaza wengine wawili ambao wataingia nao makubaliano.

Alisema hadi sasa wapo na SportPesa ambao wamewapa zaidi ya Sh250 milioni, Puma Energy ya Tanzania na Orxy Gas wote wamewapa zaidi ya Sh100 milioni kila mmoja.

Benki ya NMB waliwapatia vifaa vya michezo na Halotel ambayo ni kampuni ya simu iliwapa Sh10 milioni.

“Tunashukuru pia nguvu wanayotupatia wabunge wanaotoka Mkoa wa Singida kama Mwigulu Nchemba kwa kuweza kujitoa kwa hali na mali katika maandalizi ya timu yetu na hata kufanikisha kwa kiasi kikubwa ujenzi wa Uwanja wa Namfua ambao tutautumia kwa mechi za nyumbani msimu ujao,” alisema Festo.     

Advertisement