Singano atoa neno Mazembe

Muktasari:

Hivi karibuni, mabosi wa klabu hiyo wamemsajili mshambuliaji Eliud Ambokile kutoka Mbeya City aliyesaini mkataba wa miaka mitatu na kumnasa Singano ambaye ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Azam FC.

KLABU ya TP Mazembe ya DR Congo hadi sasa imesajili Watanzania watano ambao wamecheza kwa nyakati tofauti na juzi Alhamisi ilikamilisha usajili wa winga Ramadhani Singano huku akiahidi kupambana kufikia malengo.
Hata hivyo, nyota waliong'ara zaidi wakiwa TP Mazembe ni Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao waliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mbingwa Afrika mwaka 2015 wakati wachezaji hao mikataba yao ikielekea ukingoni.
Kwasasa Samatta anakipiga KR Genk ya Ubelgiji ambako pia anadaiwa kutaka kutimka wakati Ulimwengu yeye anaichezea JS Soura ya Algeria.
Kabla ya nyota hao wawili, Mazembe ilimsajili Ngawina Ngawina aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kuichezea timu hiyo mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Hivi karibuni, mabosi wa klabu hiyo wamemsajili mshambuliaji Eliud Ambokile kutoka Mbeya City aliyesaini mkataba wa miaka mitatu na kumnasa Singano ambaye ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Azam FC.
Singano anasema imekuwa faraja kwake kupata timu nje ya nchi na kwamba yupo tayari kupambana na changamoto mpya.
Anasema anatambua Mazembe ni klabu kubwa yenye wachezaji wazuri lakini haimkatishi tamaa kukamilisha lengo lake kama ilivyokuwa kwa wachezaji Watanzania waliowahi kupita hapo akitolea mfano wa Samatta na Ulimwengu.
"Siwezi kuwa kama Samatta ama Ulimwengu kwani kila mmoja ana kiwango chake cha uchezaji ila natamani na ninaamini nitapambana kwa kadri niwezavyo kufikia malengo yangu na ya timu, nafahamu kwamba mwanzo ni mgumu na unakuwa na changamoto nyingi.
"Siwezi kukimbia changamoto kwani ndizo humkomaza mchezaji ama mtu yoyote yule anapoamua kufanya jambo fulani, hivyo nafurahia kupata nafasi kwenye klabu kubwa kama hii ya TP Mazembe.
"Ni  jambo la kumshukuru Mungu kufika huku salama na pia Mazembe ni timu kubwa Afrika na kila mchezaji angetamani kufika hapa na kwa upande mwingne nawashukuru Watanzania wote kwa kila hatua tuzidi kuombeana kheri ili tuwe wengi nje ya Tanzania kwa  ajili ya taifa letu," anasema
Winga huyo alisema uwepo wake na Ambokile anaamini utakuwa na mchango mkubwa ndani ya timu kama ilivyokuwa kwa watangulizi wao Samatta na Ulimwengu.
"Ni furaha kuwa na mwenzangu Ambokile ambaye ni Mtanzania, ushirikiano wetu ndiyo kitu kikubwa ikiwemo kujitmbua ambapo lengo letu la kuwepo hapa ni kubwa, hatupaswi kukumbuka tulipojikwa na kuanguka, tunahitaji kufungua ukurasa mpya wa maisha mapya ya ugenini.
"Hatupaswi kukubali kukata tamaa wala kukatishwa tamaa kwa magumu na changamoto tunazopitia kwani wakati mwingine changamoto ndizo husaidia kumpa mtu mafanikio, naamini wachezaji wengi wakipata nafasi ya kucheza nje wasiogope," alisema Singano.
Singano alitua Azam FC mwaka 2015 baada ya kuvunja mkataba na Simba ambao ilidaiwa kukiuka baadhi ya vipengele vya mkataba wake ambapo mwaka 2017 alipata dili ya kuichezea klabu ya El Jadidi ya Morocco anayoichezea Mtanzania, Simon Msuva lakini mpango huo haukukamilika baada ya wakala wake kumtibulia.
Azam waliamua kurejesha kikosini na kumpa mkataba ambao umemalizika msimu uliopita.