HISIA ZANGU : Simulizi ya Chuji na Elius Gaspar Pelembe

Tuesday August 13 2019

By Edo Kumwembe

Simulizi la mastaa wawili niliowaona katika ujana wao na ubora wao Oktoba 2006 pale Maputo. Kiungo mmoja wa Msumbiji aliitwa Elias Gaspar Pelembe, lakini alijulikana zaidi kama Domingues. Alikuwa fundi sana. Alikuwa anavaa jezi namba 7.

Katika pambano dhidi ya Taifa Stars ya Marcio Maximo alikuwa hakabiki. Alikuwa anahaha uwanja mzima. Miguu yake ilikuwa myembamba kama ya Riyad Mahrez. Kuanzia hapo nikaanza kumfuatilia. Alikuwa anacheza Desportivo Maputo, baada ya mechi hiyo nikamsikia anacheza Supersport

United na kisha Mamelodi Sundowns. Sasa hivi namfuatilia tena. Ana umri wa miaka 35 na Novemba 13 mwaka huu atatimiza miaka 36.

Anakipiga katika klabu ya Bidvest Wits palepale Afrika Kusini. Bado ni mshindani. Bado anapambana. Watoto wa Uswahilini watakwambia ‘bado mtu sana’.

Hata hivyo, pambano hilohilo la Stars na Msumbiji na sisi tulikuwa na Athuman Idd ‘Chuji’. Jezi namba 4 mgongoni. Kiungo maridadi katika ujana wake na ubora wake. Chuji alikuwa na kila kitu katika soka.

Domingues alikuwa na mbwembwe zaidi za soka la mtaani, lakini Chuji alikuwa na uwezo wa kukaba, kupiga pasi fupi na ndefu, kuburuza mpira na kuuachia mbele zaidi.

Advertisement

Leo nasikia Chuji ameachwa na Coastal Union katika umri wa miaka 31. Kumbuka kwamba Domingues ana miaka 35 na bado yupo Ligi Kuu ya Afika Kusini. Hata kwao hajarudi. Chuji hakuwahi kuondoka nchini. Na hapahapa nchini hatakiwi na timu kubwa katika umri wa miaka 31.

Hawa ni wanasoka wawili tofauti waliochagua maisha tofauti. Huyu Domingues kwa vyovyote ilivyo alitambua kwamba soka ni kazi yake. Si ajabu itakuwa anajilinda, amekuwa makini na kazi yake. Ukifanya hivyo soka linakupeleka katika miaka mingi huku ukihitajika. Haishangazi kuona kwa miaka 13 anaburuza Ligi Kuu ya Afrika Kusini. Atakuwa na maisha mazuri.

Chuji, kiungo bora kama alivyo ni mwathirika wa tatizo la kutojitambua. Nyakati zile kama ilivyo nyakati hizi, wachezaji wetu wengi hawajui kwamba soka ni maisha yao. Lakini hapo hapo hawatambui kwamba soka ni mchezo wa muda mfupi.

Pamoja na hilo, kama mpira umeondoka miguuni huku ukidhalilishwa kuachwa na Coastal Union katika umri wa miaka 31, ni wazi kwamba kulikuwa na matatizo binafsi katika maisha ya Chuji mwenyewe. Ni rafiki yangu na kuna mambo mengine hayawezi kuandikwa hapa.

Hata hivyo ukweli ni kwamba katika umri wa miaka 31, kuna viungo wengi duniani wanaburuza na ni mihimili katika timu. Huu ni umri ambao mchezaji anakuwa na ukomavu wa hali ya juu katika soka. Akifikisha miaka 34 anaweza kupungua kasi na kuachia ngazi kwa kurudi katika timu za chini.

Kuna mambo mawili hapa. Kwanza kabisa, kama Chuji yule angeondoka nchini katika umri wa miaka 23, leo angekuwa anacheza soka la kiwango cha juu zaidi. Mwili wake ungekuwa fiti zaidi. Wenzetu wanakula vizuri, wanafanya mazoezi ya kishindani ambayo yanawaacha wakiwa fiti zaidi.

Kwa mfano, Mbwana Samatta au Simon Msuva wanaweza kucheza soka la kiwango cha juu mpaka wakiwa na miaka 34. Wanajua miiko ya soka. Wanaishi katika miiko ya soka. Kuanzia hapo wataanza kushuka taratibu lakini umri wa miaka 38 tuwategemee akina Samatta na Msuva wakirudi nchini kuchezea Simba na Yanga. Wakati huohuo ukumbuke kwamba leo Chuji anadhalilika na Coastal Union akiwa na miaka 31 tu.

Lakini pia ukijichanganya na wenzetu basi wanakupa akili za maisha na ushindani ambavyo vinakuonyesha kuwa miaka si lolote.

Huwa naamini wachezaji wa Kitanzania wakijenga urafiki hauwasadii sana kama ambavyo wachezaji wetu wakienda nje na kujenga urafiki na wale wa nje.

Leo Samatta rafiki yake mkubwa ni Jose Aidoo. Nilienda Genk, Mei mwaka huu, nikawakuta wakiwa wote. Sasa hivi Aidoo amenunuliwa na Celta Vigo ya Hispania. Ukiwa na rafiki wa hivi hauwezi kurudi nyuma. Lakini wote tunafahamu wachezaji marafiki wa Chuji ni akina nani.

Kama Chuji hatakiwi na Coastal katika umri wa miaka 31 basi ana mambo mengi ya kuwafundisha akina Jonas Mkude. Soka ni mchezo wa muda mfupi. Wachezaji wengi ukikutana nao kuanzia nyakati zile za Chuji hadi leo watakupiga chenga za hapa na pale na kukudanganya mengi kuhusu maisha yao ya soka lakini ukweli ni kwamba wengi wamekuwa wakipendezwa na sifa za Uwanja wa Taifa.

Kulikuwa na wachezaji wachache ambao hawakuwa na vipaji vikubwa sana vilivyopitiliza, lakini walikuwa wapambanaji wa ndani na nje ya uwanja. Mmojawao ni huyu hapa, Danny Mrwanda.

Popote alipo, afikishiwe salamu kwamba alijaribu. Anaweza kupiga hesabu zake na kusema alikuwa mwanasoka wa kulipwa.

Advertisement