Simeone kumlipa mshahara Guardiola,Klopp na chenji inabaki

Muktasari:

Taarifa zinafichua huduma yake anayotoa huko Wanda Metropolitano, inamfanya alipwe Pauni 36.2 milioni kwa mwaka kwenye mshahara wake, ikiwa ni karibu mara mbili ya kiwango anacholipwa Guardiola huko kwa matajiri Manchester City.

LONDON,ENGLAND . KUNA watu wanapiga pesa kimyakimya. Ukiulizwa hapo, kocha gani Ulaya anapiga pesa ndefu kuliko wote, haraka tu utamtaja Pep Guardiola.

Utamtaja pia Jose Mourinho, Jurgen Klopp na pengine Zinedine Zidane. Lakini, kumbe kuna mtu tofauti kabisa, ndiye anayelipwa mkwanja mrefu kwenye orodha ya makocha maarufu Ulaya.

Unajua nani? Ni yule Muargentina wa Atletico Madrid, Diego Simeone.

Shughuli yake Klopp anaifahamu vyema, juzi tu hapo Jumanne chama lake lilisambaratisha Liverpool, bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora.

Sasa Simeone ndiye kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi, akiwaacha kwa mbali wapinzani wake kwenye soka la Ulaya.

Taarifa zinafichua huduma yake anayotoa huko Wanda Metropolitano, inamfanya alipwe Pauni 36.2 milioni kwa mwaka kwenye mshahara wake, ikiwa ni karibu mara mbili ya kiwango anacholipwa Guardiola huko kwa matajiri Manchester City.

Hiyo ina maana Simeone aliyekuwa staa matata kabisa enzi zake, analipwa zaidi ya mara mbili ya mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa katika klabu hiyo. Simeone anapokea mshahara wa Pauni 700,000 kwa wiki, wakati kipa Jan Oblak, anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwa wachezaji wa Atletico Madrid, yeye anapokea Pauni 300,000 kwa wiki.

Kwa mujibu wa L’Equipe, wamechapisha orodha ya makocha wa soka wanaolipwa mshahara mkubwa, ambapo mabosi watatu wa Ligi Kuu England wameingia kwenye orodha ya makocha watano wanaolipwa pesa ndefu huko Ulaya.

Guardiola kwa sasa analipwa Pauni 20 milioni kwa mwaka pale Man City, huku mkataba wake ukifika tamati kipindi cha majira ya kiangazi mwaka 2021.

Lakini, Mhispaniola huyo mshahara wake unaweza kuongezeka kutokana na Man City kutaka abaki.

Kwa mshahara huo anaolipwa Simeone ndio maana amekuwa hana haraka ya kutaka kuachana na maisha ya Wanda Metropolitano licha ya kwamba amekuwa akikumbana na wakati mgumu miaka ya karibuni. Huko nyuma aliwahi kuhusishwa na kazi za maana kama vile kwenda kuinoa Manchester United. Mshahara wake anawaburuza makocha wote maarufu, akiwamo Mourinho na Klopp, waliopo kwenye Ligi Kuu England na vikosi vyao ya Tottenham Hotspur na Liverpool mtawalia.

Mourinho alipotua Spurs amekubali dili la kulipwa Pauni 15 milioni kwa mwaka, sawa na anavyolipwa Klopp huko Anfield baada ya kukubali dili jipya kwenye kikosi hicho cha mabingwa watarajiwa wa Ligi Kuu England. Kwenye orodha ya makocha wanaolipwa mkwanja mrefu, anayeshika namba tano ni Zinedine Zidane wa Real Madrid, ambaye kwa mwaka analipwa Pauni 14 milioni, wakati kwenye namba sita yupo, Carlo Ancelotti, anayelipwa Pauni 11.5 milionu huko Everton. Wengine ni Brendan Rodgers wa Leicester City, ambapo bosi huyo wa Ireland Kaskazini, anapokea Pauni 10 milioni kwa mwaka na anashika namba tano kwa makocha wanaolipwa vizuri Ligi Kuu England.