Simbu aibuka kivingine Kili marathoni

Friday February 28 2020

Simbu aibuka kivingine Kili marathoni,MWANARIADHA nyota nchini, Alphonce Simbu ,Kilimanjaro Marathoni ,

 

By Imani Makongoro ,Kilimanjaro

MWANARIADHA nyota nchini, Alphonce Simbu msimu huu wa mbio za Kilimanjaro Marathoni atashiriki kivingine kwa kofia ya ukocha.
Simbu ambaye ni miongoni mwa wanariadha wawili waliofuzu kushiriki Olimpiki msimu huu atakuwa miongoni mwa washiriki wa mbio za Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika keshokutwa Jumapili kwenye uwanja wa Ushirika mjini Moshi kwa kofia ya ukocha.
"Nilitamani nikimbie katika mbio hizo lakini Machi 8 nitakuwa Japan kwenye mbio za Lake Biwa Marathoni hivyo kanuni za marathon zinanibana, lakini  nitamleta mbadala wangu ambaye ni mwanariadha ninayemfundisha na ana ndoto za kufuata nyayo zangu," alisema Simbu.
Licha ya kutomtaja kwa jina mwanariadha huyo, Simbu amesema amekuwa akimfundisha mwanariadha huyo kwa muda mrefu na Jumapili atamtambulisha rasmi katika mbio za Kilimanjaro marathoni huku akiamini atafanya vizuri.
"Naamini atafanya vizuri na safari yake ya kuwa nyota wa riadha itaanzia kwenye mbio hizo atakapochuana kwenye full marathoni (kilomita 42)," alisema.
Akizungumzia safari yake ya Japan, Simbu alisema ataondoka nchini Machi 6 sanjari na kocha wake Francis John.
"Licha ya kusaka medali, pia nitazitumia mbio za Lake Biwa marathoni kupima kiwango changu kabla ya kuelekea Olimpiki 2020," alisema Simbu.

Advertisement