Simbu, Sulle wanusa dhahabu mbio za dunia Doha

Muktasari:

Simbu na Sulle ni miongoni mwa wanariadha watano waliofuzu kuiwakilisha nchi katika mbio za dunia zitakazoanza Septemba 27 hadi Oktoba 6 mjini Doha, Qatar.

Dar es Salaam.Muda wanaotumia wanariadha nyota nchini, Alphonce Simbu na Augostino Sulle umefufua matumaini ya Tanzania kuvuna medali ya dhahabu katika mbio za dunia msimu huu.

Simbu na Sulle ni miongoni mwa wanariadha watano waliofuzu kuiwakilisha nchi katika mbio za dunia zitakazoanza Septemba 27 hadi Oktoba 6 mjini Doha, Qatar.

Bingwa mtetezi raia wa Kenya, Geoffrey Kipkorir Kirui alitwaa medali kwa kutumia saa 2:08:27 muda ambao haufui dafu kwa Sulle ambaye ana rekodi ya kukimbia saa 2:07:44 akimuacha kwa sekunde 43 Kirui. Sulle aliweka rekodi hiyo katika mbio za Toronto Marathoni.

Mshindi wa medali ya shaba ya dunia Simbu, naye anapigiwa hesabu ya dhahabu msimu huu kutokana na muda anaokimbia wa saa 2:08:27 ambao ni sawa na ule wa bingwa mtetezi wa dunia kutoka Kenya. Simbu aliweka rekodi katika mbio za Lake Biwa Marathoni nchini Japan.

"Riadha bingwa anajulikana kutokana na muda wake, kwa muda wa wakimbiaji hao nafasi ya kufanya vizuri ipo," alisema bingwa wa zamani wa Madola, Gidamis Shahanga.

Mshindi wa medali ya shaba ya Olimpiki ya 1980 na kocha wa timu ya riadha ya Brunei, Suleiman Nyambui alisema ushindi wa wanariadha hao katika mbio za dunia uko mikononi mwa viongozi.

"Wanapaswa kuandaliwa kwa tofauti, kuanzia sasa wa 'focus' mbio hizo na kuanza kujiandaa, watafanya vizuri kwani muda wanaokimbia ni 'best'," alisema Nyambui.

Wanariadha wengine waliofikia viwango Stephano Huche ambaye alifuzu baada ya kukimbia kwa saa 2:12:24 kwenye mbio za Seoul marathoni, Korea na Ezekiel Ngimba aliyefuzu katika mbio za Frankfurt Ujerumani akikimbia kwa 2:13:32.

Failuna Abdi ni mwanamke pekee aliyefuzu kuiwakilisha nchi mpaka sasa ambapo alifikia viwango katika mbio za Sanlam Cape Town marathoni alipokimbia kwa saa 2:29:59.

Failuna anatarajia ushindani kutoka kwa bingwa mtetezi wa mbio za dunia raia wa Burundi, Rose Chelimo mwenye rekodi ya saa 2:27:11.