Simbu, Geay kuonyeshana ubavu mbio za Boulder

Muktasari:

Kwa upande wake Geay amesema kuwa ana matumaini ya kushinda mbio hizo kutokana na kuzifahamu vema barabara yake lakini pia amekwisha zoea mazingira.

ARUSHA.JUMLA ya wanariadha watano kutoka Tanzania wanatarajia kushiriki mbio za “Boulder to Boulder 10K” zinazotarajia kufanyika katika jimbo la Colorado nchini Marekani Mei 27 mwaka huu.

Mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka katika mji wa Boulder, wanariadha nyota kutoka Tanzania wanatarajia kuondoka leo Alhamisi kuelekea nchini humo kuungana na wanariadha wengine kutoka mataifa mbali mbali.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na habari cha RT, Tullo Chambo amewataka wanariadha hao kuwa ni Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Josepha Panga ambao wataongozana na Magdalena Shauri na Natalia Elisante.

“Timu iko kamili na itaondoka kesho mchana (leo) kuelekea katika mji huo wa Boulder kwa ajili ya kutuwakilisha katika mbio hizo za umbali wa 10K ambayo mwanariadha Geay amekuwa na bahati kwenye mvbio hizo,” alisema Tullo

Kwa upande wake Geay amesema kuwa ana matumaini ya kushinda mbio hizo kutokana na kuzifahamu vema barabara yake lakini pia amekwisha zoea mazingira.

“Mimi tiyari niko huku Marekani tangu wiki iliyopita nilipokuja kushiriki mbio za “Alaska airlines bay to breaker 12k” zilizomalizika jumatatu na nimeshinda nafasi ya kwanza ambayo ushindi umetokana na kuzoea mazingira na hali ya hewa”

Kwa upande Simbu amesema anakwenda kushiriki akijua macho mengi ya watanzania yanamtazama yeye hivyo atakimbia kizalendo kuhakikisha anairejesha heshima yake katika mbio.

“Kikubwa watanzania watuombee uzima na afya na sisi tutarudisha fadhila hizo kwa kuijulisha dunia kuwa Tanzania ipo na ina vipaji vya riadha”