Simba yawapa raha mashabiki ikiiua JS Saoura mabao 3-0

Saturday January 12 2019

 

By ELIYA SOLOMON

Timu ya Simba imeibuka na ushindi mnono baada ya kuilaza JS Saoura mabao 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere (2) yameifanya timu hiyo kuongoza Kundi D.

Awali, dakika 45 za kipindi cha kwanza za Simba SC ilikwenda mapumziko ikiwa inaongoza  bao 1-0 lililofungwa mwishoni na Emmanuel Okwi.

Mganda Juuko Murshid alionekana kufiti kwenye nafasi ya Erasto Nyoni ambaye ni majeruhi kwa kucheza kwa maelewano mazuri na Paschal Wawa ambaye ni kama kiungozi kwenye safu ya ulinzi ya Simba.

Mabeki hao walikuwa wakifanya kazi ya ziada kwa kuwasaidia walinzi wa pembeni wa Simba pindi ambapo walikuwa wakishindwa kuwadhibiti washambuliaji wa JS Saoura.

Safu ya ulinzi ya Simba SC ilikuwa ikiundwa pia na kina Nicholus Gyan na Mohammed Hussein 'Tshabalala'.

Mabeki wa kati,  Pascal Wawa na Juuko Murshid walionekana kuwa na maelewano mazuri kwenye kikosi cha Simba.

Advertisement