Simba yatua na sapraizi hii kwa Azam FC

Tuesday June 30 2020
yanga pic

MABINGWA mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba waliwasili Dar es Salaam jana saa 6:30 mchana kwa ndege wakitokea Mbeya, lakini wamewaandalia Azam FC sapraizi saba kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba jana hawakuwa na shamrashamra zozote kwenye Uwanja wa Ndege wala mitaani kusheherekea ubingwa wao kwani wamesisitiza watafanya hivyo baada ya kumaliza mechi ngumu ya kesho dhidi ya Azam kwenye robo-fainali ya Kombe la Shirikisho.

Simba ambao tayari wana uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wanataka kubeba na Kombe la Shirikisho ili kuweka heshima.

Lakini Azam huenda wakakumbana na sapraizi za sura saba mpya kwenye kikosi cha kwanza ambazo zilipumzishwa kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Prisons kwani haikuwa na umuhimu mkubwa kama ya Shirikisho ambayo ni pata potea.

Wachezaji hao saba ambao wataanza dhidi ya Azam ni nahodha John Bocco, Clatous Chama na Luis Jose Miquissone ambao waliingia kipindi cha pili kwenye mechi ya Prisons wakati Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa na Francis Kahata hawakucheza kabisa ili kutunza nguvu.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema mechi ya Prisons walifahamu fika wanakwenda kucheza mechi ngumu ndio maana hata matokeo yake yalikuwa suluhu lakini walihifadhi nguvu ya kutosha kwa ajili ya robo fainali dhidi ya Azam.

Advertisement

“Ukiangalia Simba haina historia nzuri katika FA, kwa misimu miwili mfululizo kutolewa mapema kwa maana hiyo msimu huu tumelitolea macho FA na tunataka kufanya vizuri kwa kulichukua ndio maana kuna baadhi ya wachezaji niliwapumzisha hawakucheza kabisa,” alisema.

“Kutafuta pointi moja katika michezo saba (ili kuwa mabingwa wa Ligi Kuu) tulifahamu ingepatikana tu, lakini kama tukishindwa kufanya maandalizi mazuri ya umakini mkubwa kwa mechi na Azam tukifungwa tutakuwa tumeondolewa katika mashindano jambo ambalo hatutamani litokee,” alisema Sven.

Kukosekana kwa wachezaji hao saba nafasi zao zilichukuliwa na Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga, Miraji Athumani na Mzamiru Yassin ambao walifanya vizuri.

Bocco alisema matokeo ambayo waliyapata katika mechi mbili za Mbeya wameshayasahau na akili zao sasa zipo katika mchezo unaofuata dhidi ya Azam.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema; “Kutakuwa na motisha kama watashinda mechi hiyo, kwa maana hiyo jukumu na masuala mengine ya kiufundi yamebaki kwao.”

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alitamba kwamba watatwaa taji la Ligui Kuu hata mara kumi mfululizo kwani wana uwezo na hawatakuwa na shamrashamra zozote hadi baada ya mechi yao kesho.

Advertisement