Simba yashtukia janja CAF

Muktasari:

  • Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema wameshindwa kufanya usajili katika dirisha dogo la CAF kutokana kikosi chao kuwa na idadi kamili ya wachezaji wanaotakiwa kuwatumia, lakini pia kalenda ya TFF imewakwamisha kiaina kufanya usajili mpya

NYOTA wa kikosi cha kwanza cha Simba kimerejea Dar es Salaam na kupishana na wadogo zao wa U20 waliokwenda Zanzibar kushiriki mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, huku mabosi wa klabu hiyo wakishtukia jambo na fasta kuishtua TFF.

Benchi la ufundi lote la Simba na wachezaji wao 18 wamerejea kwa ajili ya mechi yao ya keshokutwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria, lakini kuna kitu wakalishtukia na kama TFF halitalifanyia kazi itazingharimu timu za Tanzania.

Kalenda ya usajili ya Shirikisho hilo la soka Tanzania, haliendani na lile la Shirikisho la Afrika (CAF) na kusisitiza ndio inayowabana hata sasa kufanya usajili kwenye dirisha la usajili ya Ligi ya Mabingwa.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema wameshindwa kufanya usajili katika dirisha dogo la CAF kutokana kikosi chao kuwa na idadi kamili ya wachezaji wanaotakiwa kuwatumia, lakini pia kalenda ya TFF imewakwamisha kiaina kufanya usajili mpya.

Try Again alisema kama wangekuwa na mpango wa kuongeza nguvu katika timu yao kwa kusajili nyota mwingine ilikuwa lazima wamuache mmoja, ambaye yupo katika usajili wa CAF jambo ambalo lilishindikana kutokana wachezaji wote waliopo kwa sasa ni muhimu na wako kwenye mipango ya kocha katika mshindano hayo.

Anasema jambo lingine ni kipindi cha usajili wa CAF tayari Tanzania huwa umeshafunga na kushindwa kupenyeza mchezaji mpya kirahisi.

“Kama kipindi cha usajili wa CAF unaendana na wa TFF ingekuwa vizuri kwetu kwani, hata kama tungeshindwa kumtumia mchezaji huyo katika michuano ya kimataifa, tungemtumia katika ligi,” alisema.

“Tumekaa na kuzungumza na TFF ili kuona jinsi gani wanaweza kuliona hili na wakalifanyia mabadiliko ili usajili wa sehemu zote mbili uende sambamba hata kama ukimsajili mchezaji mpya anakuwa na uwezo wa kumtumia kokote.

“Tunashukuru TFF wamelipokea vizuri hili na wameliona litakuwa na manufaa kwa ligi ya ndani na timu ambazo zinacheza michuano ya kimataifa na wametuahidi watalifanyia kazi,” alisema Try Again.

KIKOSI CHARUDI

Kikosi cha Simba kiliwasili jana Jumatano kikiwa na nyota 18 waliokuwa kwenye Kombe la Mapinduzi na watafanya mazoezi ya siku mbili kuanzia leo Alhamisi kabla ya Jumamosi kuvaana na JS Saoura.

Wachezaji waliotua ni John Bocco, Aishi Manula, Shiza Kichuya, Meddie Kagere, Nicolas Gyan, Pascal Wawa, Clatous Chama na Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, James Kotei na Deogratius Munishi ‘Dida’. Wengine ni Hassan Dilunga na Juuko Murshid, Rashid Juma, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Jonas Mkude.

Wakati hao wakirejea Dar, vijana wa U20 pamoja na kocha wao, Nico Kiondo walitua Zanzibar tayari kwa mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo itakayochezwa kesho Ijumaa. Simba na KMKM zilifuzu kutoka Kundi A, huku Azam na Malindi zikipenya kutoka Kundi B.