Simba yarahisishiwa kazi Kitwe

Muktasari:

SIMBA ndio inayoshikilia rekodi kwa klabu za Tanzania kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika, kwani iliwahi kufika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) mwaka 1974 na kucheza fainali za Kombe la CAF 1993.

Dar es Salaam. KIKOSI cha Simba kimetua salama nchini Zambia na jioni ya jana kilifanya mazoezi kwenye uwanja wa wapinzani wakubwa wa Nkana FC,  Power Dynamos mjini Kitwe.

Viongozi wakuu wa Simba sambamba na wale wa klabu Dynamos walikuwa wakijadiliana mambo mbalimbali kwa furaha wakati mazoezi hayo yakiendelea chini ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems na wasaidizi wake.

Kupokewa kwa Simba na wapinzani wa Nkana, Dynamos ni kama kuwarahisishia kazi kwenye mchezo wao wa awali wa raundi ya kwanza ta Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao kabla ya kurudiana nao wiki moja baadaye jijini Dar.

.

Simba iliondoka alfajiri ya jana kwenda Zambia na ilitua mjini wa Ndola kabla ya kuunga tena mpaka Kitwe na kupokewa kwa shangwe na Watanzania waliopo nchini humo tayari kwa mchezo wao utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nkana, mjini Kitwe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, nyota wote 20 waliosafiri na timu hiyo wapo vizuri tayari kwa mchezo huo, huku benchi la ufundi la Simba likisisitiza limefuata ushindi katika pambano hilo.

Simba inakutana na Nkana kwa mara ya tatu mjini Kitwe, huku ikiwa na rekodi mbaya ya kupoteza mechi zote mbili za awali walizocheza na wapinzani wao katika michuano hiyo ya Afrika.

Mara ya kwanza walikutana mwaka 1994 na katika hatua ya robo fainali na Simba ilicharazwa mabao 4-1 kabla ya kuja kulipa kisasi jijini Dar es salaam kwa ushindi wa mabao 2-0 na kung'olewa kwa jumla ya mabao 4-3.

Mara ya mwisho walivaana tena katika mechi za raundi ya kwanza na Simba ililala ugenini mjini Kitwe kwa mabao 4-0 kabla ya kulipiza kisasi tena nyumbani ikiinyuka  Nkana 3-0, lakini hayakuisaidia kwa vile mnyama alitolewa kwa jumla ya mabao 4-3.