Simba yaokota dodo kwa Onyango

Wednesday August 12 2020

 

By MWANDISHI WETU

GOR MAHIA imethibitisha kupitia mtandao wao imeshindwa kumzuia beki wao tegemeo, Joash Onyango asijiunge na Simba kutokana na ishu ya fedha.

Beki huyo ambaye amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii kutokana na ubishi juu ya umri wake wa miaka 27, takwimu za pasi yake ya kusafiria zinaonyesha amezaliwa 1993.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa soka la Kenya, Simba imeokota dodo kutokana na umahiri na uzoefu wa mchezaji huyo kwani mkataba wake na Gor Mahia ulishamalizika na anatua Msimbazi kama mchezaji huru jambo litakalowapunguzia Simba gharama.

Wanasema mchezaji huyo si Babu kama wanavyotafsiri mashabiki wa Bongo kwani, ni staili yake ya kawaida ya kupaka rangi ndevu.

Gor Mahia imeandika kwenye mtandao huo kuwa Onyango huenda akasaini dili ya miaka miwili muda wowote kuanzia sasa kwa kuwa wameshaafikiana kuhusu maslahi binafsi.

Onyanyo, ambaye ni beki tegemeo kwenye timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars alijiunga na Gor Mahia mwaka 2017 akitokea Western Stima na kushinda mataji kadhaa.

Advertisement

Msimu wa 2018/19 alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu.

Gor wameshindwa kumzuia kutokana na hali ngumu ya fedha iliyopo klabu hapo kwa sasa.

Onyango anajiunga na Meddie Kagere na Francis Kahata ambao, walicheza pamoja Gor Mahia.

Onyango alipoulizwa jana aligoma kufafanua lolote kuhusu dili lake na Simba kwa madai bado hajakamilisha baadhi ya mambo. Simba ambao jana walikuwa bize wakihangaika na hukumu ya Bernard Morrison, wanasuka upya safu yao ya ulinzi kujiweka sawa kwa Ligi ya Mabingwa Afrika baadaye mwaka huu.

Advertisement