Simba yamuibua Shahanga

Muktasari:

Shahanga mbali na kukoshwa na kiwango cha Simba, ameelezea namna ambavyo Tanzania inachelewa kuandaa timu kwa ajili ya michezo ya Afrika (All African games).


ACHANA na kipigo cha mabao 5-4 ambacho Simba iliambulia juzi Alhamisi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Sevilla inayoshiriki Ligi ya Hispania, kiwango walichoonyesha nyota wa Simba kimemuibua nyota wa riadha nchini, Gidamis Shahanga.

Shahanga aliyefunguka kuwa yeye ni shabiki wa Simba ambaye alianza kuishabikia timu hiyo baada ya kukoshwa na kiwango cha Abdallah Kibaden enzi hizo, alisema kule kwao Katesh mkoani Manyara kuna watu waliamini Simba hawawezi kupata bao hata moja katika mchezo huo.

“Ilichokifanya Simba ni cha tofauti, imecheza mpira pamoja na kufungwa, kitendo cha kufunga mabao manne sio jambo dogo.

“Hata Sevilla watakuwa hawaamini walichokutana nacho pamoja na kwamba wameshinda lakini wameondoka na historia,” alisema Shahanga, bingwa mara mbili wa Michezo ya Jumuiya ya Madola katika miaka ya 1978 na 1982.

“Walisema Simba haiwezi kupenya ngome ya ulinzi ya Sevilla, lakini soka walilocheza limeonekana, hakuna ubishi kiwango cha Simba kisoka kinazidi kuimarika,” alisema.

Shahanga mbali na kukoshwa na kiwango cha Simba, ameelezea namna ambavyo Tanzania inachelewa kuandaa timu kwa ajili ya michezo ya Afrika (All African games).

Michezo hiyo itaanza Agosti 19 mwaka huu mjini Rabat, Morocco ambapo Tanzania itawakilishwa na timu za riadha, judo na soka la wanawake.