Simba yamshtua Kocha

Muktasari:

KOCHA mzoefu, Mlage Kabange ameiangalia Simba ilivyocheza mechi mbili katika viwanja vya mikoani na kuionya isipojiangalia msimu huu ubingwa watausikia kwenye bomba.

KOCHA mzoefu, Mlage Kabange ameiangalia Simba ilivyocheza mechi mbili katika viwanja vya mikoani na kuionya isipojiangalia msimu huu ubingwa watausikia kwenye bomba.

Simba ilianza ligi kwa kuifunga Ihefu SC mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Katika michezo yote mwili Simba haikucheza kwa kiwango kizuri huku wachezaji hasa wa kigeni wakiongozwa na Clatous Chama wakilalamikiwa ubovu wa viwanja.

Kabange alisema; “Nimeangalia walivyocheza hasa hawa wachezaji wa kimataifa unaona kabisa hawaonyeshi bidiii kwa kuathirika na viwanja walivyocheza.

“Sasa unajiuliza, hawavijui kuwa viwanja ni vibovu wakati wengi walichezea hivyo hivyo msimu uliopita.Lazima wabadilike wajue kuwa wanatakiwa kujituma kila mechi kulingana na viwanja vilivopo.

“Wasing’are uwanja wa Taifa tu lazima wajue kuwa msimu huu Simba lazima ikutane na wakati mgumu uwanjani kwa sababu kwanza timu nyingi zitawakamia kwa sababu ni mabingwa na kila timu inataka ubingwa pia wakiwemo wapinzani wao Yanga hivyo haitakuwa ligi nyepesi lazima wapambane kila mchezao bila kujali wanacheza kwenye uwanja gani”, alisema Kabange.

Kabange pia ameipa tano Yanga kwa usajili iliofanya msimu huu kwa kusema wameonyesha hawana utani safari hii na wanautaka ubingwa kwa hali yoyote.

“Yanga safari hii iko vizuri na hata usajili wao umeonyesha kabisa kuwa kuna kitu wanakitaka, hivyo msimu huu kazi itakuwepo”, alisema Kabange.