Simba yamponza mwamuzi, TFF yamshushia rungu Nsajingwa

Muktasari:

Shadrack Nsajigwa amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini laki tano baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi

KOCHA msaidizi wa Singida Utd, Shadrack Nsajigwa amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini laki tano baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kupinga maamuzi ya Mwamuzi.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam kwamba Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Kocha wa makipa wa African Lyon, Juma Bomba amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kupinga maamuzi ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Katika kikao hicho pia mtunza vifaa wa Ruvu Shooting, Augustine Palangwa anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwa Waamuzi kwenye mchezo namba 167  Desemba 16, 2018: Yanga 3 na Ruvu Shooting 2.
Klabu ya Singida Utd imetozwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kutokana na timu yake kutoingia kwenye chumba cha kubadilishia (changing room), na badala yake kuingia kwenye chumba cha waandishi wa habari, jambo lililosababisha usumbufu kwa waandishi wa habari. Adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Klabu za Mbao na Alliance FC zimepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kila moja kwa kushindwa kuingiza timu za U20 kwenye mechi ya utangulizi. Faini hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 71(2)(a) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Vijana na Watoto.
Pia Alliance FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia, hivyo kufanya timu yao ikaguliwe nje ya vyumba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Biashara Utd 0 vs Singida Utd 0. Mchezaji wa Singida Utd, Godfrey Mwashiuya amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga mpinzani wake ngumi kwa makusudi wakati mpira ukiwa umesimama. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mchezaji wa Singida Utd, Rajab Zahir amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuoneshwa kadi nyekundu mara baada ya mchezo kumalizika kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi na kutaka kumpiga. Adhabu hiyo imezingatia Kanu ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
JKT Tanzania 0 vs Simba 2. Mwamuzi Msaidizi namba mbili Mashaka Mwandembwa amefungiwa miezi mitatu kwa kushindwa kutafsiri vizuri sheria ya kuotea. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39 ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi. Pia Mwamuzi Mbaraka Rashid amepewa onyo kwa kutokuwa makini wakati wa akichezesha mechi hiyo.
Klabu ya Green Warriors imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wa timu yao kufanya vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Pia klabu hiyo imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na baadhi ya washabiki wao wakiongozwa na benchi la ufundi kuwazonga waamuzi huku wakiwatolea lugha chafu na kutaka kuwapiga baada ya mchezo kumalizika. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwa ndani ya uzio unaotenganisha wachezaji na washabiki kwa muda wote wa mchezo, licha ya kutakiwa kuondoka. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mchezaji wa Mgambo Shooting, Dunstan D. Lipinga (jezi namba 30) anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga Mwamuzi baada ya mchezo kumalizika. Pia mchezaji Rashid A. Shilla wa Mgambo (jezi namba 19) anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kumpiga Meneja wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Klabu ya The Mighty Elephant imepewa Onyo Kali kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo (technical meeting) bila kutoa taarifa yoyote kwa Kamishna. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Pia The Mighty Elephant imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Utaratibu wa Mchezo.

Mechi namba 18- Novemba 18, 2018: Kitayosce 0 vs Kilimanjaro Heroes 0. Kocha wa Kitayosce, Hamad Haule amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kosa la kuongea na simu hata baada ya kukatazwa na Mwamuzi wa Akiba. Adhabu imezingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Pia Mtunza Vifaa wa Kilimanjaro Heroes, Noel Paul anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kosa la kuongea na simu, licha ya kukanywa asitumie simu lakini alikaidi.

Mechi namba 27- Januari 5, 2019: Kitayosce 1 vs Mtwivila 1. Kocha wa Mtwivila, Lisa Mwalupindi amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga mwamuzi ya Mwamuzi. Adhabu imezingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Naye Daktari wa Kitayosce, Michael Evarest anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kuchelewesha kuanzishwa kwa mchezo baada ya kuamriwa na Mwamuzi atokee sehemu ya karibu alikaidi na kutokea sehemu ya mbali.

Bulyanhulu 0 vs Kasulu Red Star 0. Meneja wa Kasulu Red Star, Kapama Kapama anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi.

Milambo vs Madini SC. Timu ya Madini SC imeshushwa madaraja mawili kwa kutofika uwanjani. Hivyo, matokeo ya mechi zote ilizocheza yamefutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye Ligi.

Pia timu hiyo imepigwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili). Adhabu hizo zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 28 (1) na (2) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Kutofika Uwanjani.

Klabu ya Changanyikeni imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wa timu yao kumpiga Mwamuzi huku wakimtolea lugha ya matusi. Adhabu imezingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mmiliki wa timu ya Changanyikeni, Omar Bawazir anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kuingia uwanjani na baadhi ya washabiki na kumpiga Mwamuzi.

Vilevile Mwamuzi wa mechi hiyo, Ibrahim Mohamed ameondolewa kwenye Orodha ya Waamuzi wa SDL baada ya kupata alama za chini.

African Sports 0 vs Forest 2. Malalamiko ya African Sports kuwa usajili wa wachezaji Timotheo Emmanuel Kombo na Lawrence Milton Mganga wa Forest si halali yamekataliwa. TFF imethibitisha kuwa wachezaji hao wamesajiliwa kihalali kwenye timu ya Forest.