Simba waikimbia Singida United Dar es Salaam waenda Morogoro

Saturday January 13 2018

 

By DORIS MALIYAGA

KIKOSI cha Simba kimelihama jiji la Dar es Salaam na kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya kambi ya siku mbili kabla ya kukutana na Singida United Alhamisi ijayo kwenye  Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, lakini wageni wao wamesema watakomaa hapa na watawafunga.
Simba imeondoka asubuhi ya leo Jumamosi kwa usafiri wa basi kwenda mkoani hapo, wamefikia katika hoteli moja ambayo hawakutaka kuitaja jina, lakini wanategemea kufanya mazoezi yao kwenye uwanja wa chuo cha Baptiste.
Lakini sasa, wakati Simba wanalikimbia jiji la Dar es Salaam, wageni wao kikosi cha Singida wameweka kambi hapa na wanaendelea na mazoezi yao kama kawaida Uwanja wa Karume.
Kocha mkuu wa Singida United, Hans Pluijm amesema, wao wataendelea na maandalizi yao hapa Dar es Salaam na malengo yao ni kupambana na kushinda mchezo huo.
"Tunaendelea na maandalizi yetu hapa Dar es Salaam kama kawaida. Simba kuhama mji kwangu si muhimu, muhimu ni kuandaa timu yangu kwa ukamilifu,"anasema Pluijm kocha wa zamani wa Yanga.
Pluijm ambaye ni Mholanzi alienda mbali na kusema: "Inawezekana wao wameona kuandaa timu nje ya mji ni nzuri zaidi, hayo ni mawazo yao."