Simba yajibu mapigo ya Yanga

Simba imeendeleza ubabe wake katika Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga JKT Tanzania kwa mabao 4-0 katika mechi ya raundi ya tano iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Simba ikicheza soka tamu, huku kiungo mshambuliaji wake, Luis Miquissone akiupiga mwingi na kufunga bao la kideoni wakati wakiisulubu maafande hao kwa mabao 4-0 na kurejea kileleni.

Wekundu hao wa msimbazi mechi ijayo watacheza na Yanga Oktoba 18 kwenye dimba la Mkapa kwa ushindi huo  ni kama wametuma salamu kwa watani wao wa jadi walioshinda mabao 3-0 jana dhidi ya Coastal Union.

Kocha Sven Vandenbroeck kwa mara ya kwanza leo aliwatumia washambuliaji wawili, Meddie Kagere na Chris Mugalu kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu wa kutumia straika mmoja.

Licha ya ubovu wa Uwanja wa Jamhuri, haikuwazuia Simba kushinda na kupiga mpira wao wa kuvutia na kuwapa burudani mashabiki wa soka waliofurika kwenye uwanja huo.

Simba ilionyesha kuwa na kiu ya ushindi na kutaka kulipa kisasi cha kufungwa na JKT kwenye mechi yao ya mwisho ya msimu uliopita walipotunguliwa 1-0 nyumbani jijini Dar es Salaam kwani ilianza kwa kasi na iliwachukua dakika nne tu Kagere kufunga bao kwa kichwa akimalizia krosi ndefu ya kiungo Larry Bwalya likiwa ni shambulizi la pili kwao kulifanya kwenye lango la JKT.

Wakati JKT wakijiuliza jinsi ya kurejesha bao hilo, Mugalu alifunga kwa kichwa tena dakika mbili baadaye akimalizia krosi ndefu ya Luis, likiwa bao la tatu kwake katika mechi tatu alizocheza katika ligi akilingana na Prince Dube wa Azam ambaye usiku alikuwa na kazi dhidi ya Kagera Sugar.

Dakika ya tisa JKT walirudi mchezoni na kufanya mashambulizi mazuri la kwanza beki Nurdin Mohamed anapiga shuti kumalizia mpira wa adhabu wa Michael Aidan na kugonga mwamba kisha mabeki wanaokoa na kuwa kona kisha kona tena na Idan ikamkuta Frank Nchimbi lakini kipa Aishi Manula anasimama vyema na kuudaka.

Licha ya JKT kucharuka, lakini wageni wao waliendelea kutawala mchezo na kuendelea kuwasumbua mabeki wa maafande hao na dakika chache kabla ya mapumziko, Kagere aliongeza bao jingine likiwa la nne kwake msimu huu. Mabao hayo yamemfanya Kagere kufikisha jumla ya mabao 49.

Kagere alifunga bao hilo dakika ya 41 kwa shuti kali la mguu wa kushoto akipokea pasi ya kiungo Clatous Chama ambaye ushirikiano wake na Luis na Bwalya uliifanya Simba ionekane kama ndio waliokuwa nyumbani na JKT wanacheza ugenini.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji na kuonekana kuwanufaisha zaidi Simba iliyopata bao la nne dakika ya 54 kupitia kwa kimiani na Luis kwa shuti kali la mbali nje ya eneo la hatari lililojaa moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa Patrick Muntary aliuangalia mpira ukijaa wavuni. Luis alipokea mpira huo uliokolewa na mabeki wa JKT na kufanya maamuzi ya haraka ya kuachia kombora lililotinga wavuni.

Kuingia kwa bao hilo kukamfanya Kocha Abdallah Mohmmed 'Bares' kumtoa Richard Maranya na kumuingiza Danny Lyanga, mabadiliko ambayo yaliongeza kidogo uhai wa safu ya ushambuliaji ya JKT.

Kwa matokeo hayo yaliifanya Simba kufikisha pointi 13 na mabao 14.