Simba yaiponza Yanga yapigwa faini ya Sh8 milioni

Monday March 11 2019

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Kikosi cha Yanga kimetozwa faini ya jumla ya Sh 8milioni kutokana na makosa mbalimbali waliyofanya katika mechi zao huku Simba ikipigwa faini Sh 3mil.

Yanga imekutana na lungu la kulipa kiasi hicho cha fedha ambapo Sh. 6mil ni kutokana na mchezo wao wa mzunguko wa pili dhidi ya Simba, shilingi laki tano na Mbao FC na Sh1.5 milioni dhidi ya JKT Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu, Boniface Wambura amesema Yanga wametozwa faini hiyo kwenye mechi na Simba kwa makosa ya kutotumia mlango usio rasmi wakati wa kuingia uwanjani, kwenye vyumba vya kubadilishio nguo na kwenye kiwanja.

"Simba wao wametozwa kiasi hicho cha Sh 3mil kwa sababu kosa lao ni kutumia mlango usio rasmi, Yanga wao walifanya makosa tofauti,"alisema Wambura.

Amesema, adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni na ametoa onyo kwa wanaokiuka taratibu zinazowekwa kwa sababu mashindano hayo yanaendeshwa na wadhamini kama televisheni sasa kama wanafanya kivyume haipendezi.

Wambura amesema Azam FC pia imetozwa kiasi cha Sh. 3mil kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mchezo wao dhidi ya Simba.

Advertisement