Simba yaendeleza sherehe yaipiga mkono Yanga Ligi ya Wanawake

Friday July 10 2020

 

By MWANDISHI WETU

TIMU ya wanawake ya Simba Queens imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake baada ya kuwafunga watani wao Yanga Princess mabao 5-1, mechi hiyo imepigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Awali kabla ya mchezo huo, Simba Queens ilishushwa hadi nafasi ya pili baada ya matokeo ya jana Alhamis JKT Queens iliposhinda bao 2-1. Hivyo Simba imepanda kileleni ikifikisha pointi 38 ikiwa imecheza mechi 15 mpaka sasa.
Mchezo huo unakuwa ni wanne mfululizo kwa Yanga Princess kupoteza mbele ya Simba, baada ya msimu uliopita kukubali kufungwa mabao 7-1 katika mchezo wa kwanza.
Mchezo wa pili wakapigwa bao 5-1 na mchezo wa mzunguko wa kwanza wa msimu wakafungwa bao 3-1.
Mchezo wa leo Ijumaa ulianza saa 9:30 mchana,  Yanga ilionekana kulisakama vilivyo lango la Simba, lakini kibao kilibadilika dakika 10 baadaye pale Simba walipolishambulia zaidi lango la Yanga na baada ya muda mashambulizi yakawa ni ya kupokezana.
Simba Queens ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Mwanahamisi Omary 'Gaucho' ambaye alipiga mpira kupitia upande wa kulia wa lango la Yanga ambao ulimshinda mlinda mlango na  Simba ikaandika bao la kwanza dakika ya 31.
Baada ya kuruhusu bao, Yanga walionekana kutulia na kucheza mpira wa kuonana kwa kupiga pasi fupi fupi kuanzia eneo lao la ulinzi hadi kwenye lango la Simba.
Mpango kazi huo ulikuwa na faida kwani, dakika 38, Yanga ilisawazisha bao kupitia kwa mshambulaji wake Shelda Boniphace.
Dakika ya 73, Oppah Sanga, aliipatia Simba bao la pili baada ya kupiga kichwa kilali.
Simba iliendelea na mashambulizi ambayo yalionekana kuwa na faida kwani dakika ya 73, kiungo kutoka Burundi, Joelle Bukuru alipiga shuti kali baada ya kulisakama lango la Yanga kwa dakika zipatazo tano.
Simba iliendelea na mashambulizi hadi kufikia dakika ya 80 ambapo Mwanahamisi aliifungia Simba bao la nne, kabla ya Oppah naye kupigilia msumari mwa mwisho na kufanya ubao usome  5-1 hadi mchezo ulipomalizika.
Kwa matokeo hayo, Yanga inabaki na alama zake 20 ikiwa imecheza mechi 15 na kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Mchezo ujao Yanga atacheza dhidi ya Panama Girls huku Simba akisafiri hadi  Mwanza kucheza na Marsh Queens.

Advertisement