Simba yafunguka kuhusu Tshishimbi

Dar es Salaam. Mmoja wa vigogo wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope amesema klabu hiyo haikumjadili Papy Tshishimbi kwenye usajili wao kwa kuwa walifahamu ana mkataba na timu nyingine.

Hanspope alisema pamoja na kwamba hawakuwahi kumjadili, lakini kama kocha atampendekeza katika ripoti yake wanaweza kumsajili.

Kauli ya Hanspope imekuja siku kadhaa baada ya nahodha huyo kumaliza mkataba wake na Yanga, ambayo ilitaka kumuongezea mkataba wa miaka miwili, lakini wakashindwana.

Tshishimbi, ambaye ametajwa katika orodha ya wachezaji 14 wanaoondoka Yanga, yuko mbioni kwenda kwao DR Congo kwa mapumziko ya mwisho wa msimu.

“Malengo yangu hayako timu moja, naweza kucheza timu yoyote ile hata Simba, ili mradi tuelewane na waonyeshe nia ya kunihitaji,” alisema Tshishimbi alipoulizwa juu ya mwelekeo wake.

Hata hivyo Hanspope jana alisema kuwa watahitaji kupitia kwanza ripoti ya kocha wao kabla ya kujua nani na nani wataongeza nguvu kwenye kikosi cha mabingwa hao.

Simba imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfulilizo msimu huu.