Simba yafumua usajili Yanga

Muktasari:

Yanga inataka kuwa na kikosi cha maana msimu ujao na kitakachokuwa na sura ya kuaminika katika kurejesha heshima ambayo sasa imefifia kwa msimu wa tatu mfululizo.

JANGWANI kumekucha. Unaambiwa hivi, kile kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa watani wao, Simba bado kinapasua vichwa vya mabosi wa Yanga na hata wadhamini wao na sasa hatua mpya ni hata usajili wao umeanza upya kwa kuangaliwa mara mbili.

Yanga inataka kuwa na kikosi cha maana msimu ujao na kitakachokuwa na sura ya kuaminika katika kurejesha heshima ambayo sasa imefifia kwa msimu wa tatu mfululizo.

Katika hesabu hizo, Yanga imefumua maeneo mawili ya usajili wao na kuna uwezekano mastaa wao wawili waliokuwa wanasubiri kutua klabuni hapo wakayeyuka.

ERICK RUTANGA v MUSTAPHA KIIZA

Yanga ilikuwa kama imeshamalizana na beki Mnyarwanda Erick Rutanga ambaye alitakiwa kuja kuziba nafasi ya beki ya kushoto ya kikosi chao lakini sasa mambo yamegeuka.

Mabosi wa Yanga wamerudi kwa kasi kwa beki Mustapha Kiiza ambaye ndio alikuwa chaguo la kwanza kwa ajili ya msimu ujao.

Kurejea kwa Yanga kwa Kiiza ni kutokana na beki huyo dili lake la kutua nchini Afrika Kusini kubuma na mwenyewe ndio amewashtua vigogo wa GSM wafungue mazungumzo kwa nafasi ya pili.

Kiiza ndio silaha ya kwanza ambayo Yanga wanaihitaji, lakini changamoto kubwa kwa beki huyo kushindwana na Yanga ni juu ya dau la usajili akitaka Dola 50,000 (Sh115 milioni).

Kinachowaumiza Yanga ni Kiiza ana faida kubwa katika ujuzi wake wa mguu wa kushoto na urefu wake wa kutosha katika kukabiliana na mipira ya juu.

Endapo Yanga itakubaliana na Kiiza haitashangaza kusikia wameachana na Rutanga ambaye tayari alikuwa anasubiri kujiunga na timu hiyo.

JAMES KOTEI NJE

Mghana James Kotei naye hatovaa jezi za timu hiyo baada ya mabosi wa Kamati ya Utendaji kutilia shaka usalama wa kiungo mkabaji huyo akiwa ndani ya kikosi chao.

Aliyetibua dili la Kotei ni raia mwenzake wa Ghana, winga Bernard Morrison kwani Mwanaspoti linafahamu usumbufu wa Mghana huyo ambaye anatajwa kushirikiana na baadhi ya vigogo wa Simba na hilo limewatibua Yanga.

“Kama Morrison ambaye alikuwa haijui Simba ametusumbua hivi, itakuaje huyo Kotei ambaye aliwahi kuwa huko kwa miaka kadhaa, tumewaambia GSM waachane kabisa na wachezaji ambao wameingia Simba,” alifichua kigogo mmoja wa kamati ya utendaji (jina tunalo).

Mapema bosi wa GSM, Mhandisi Hersi Said aliwahi kuliambia Mwanaspoti hawana hesabu za kuchukua staa yeyote ndani ya Simba.

Msimamo huo pia ukamnyima fursa hata staa Deo Kanda ambaye bosi mmoja wa TP Mazembe Mwanaspoti linafahamu mapema wiki moja iliyopita jina lake lilipelekwa kwa matajiri wa GSM, lakini msimamo huo ukazuia dili hilo.

Kupotezewa kwa Kotei kumeifanya Yanga kuingia vitani kusaka kiungo mkabaji mwenye uwezo bora zaidi atakayekuja kuungana na Mkongomani Papy Tshishimbi.

Harakati hizo pia ndio zilizositisha mkataba wa kiungo Mnyarwanda Ally Niyonzima ambaye hatua ya kuhitaji Dola 60,000 (Sh 138 lilioni) liligomewa na mabosi wa Yanga wakisema kiungo huyo hana thamani hiyo na kumwacha aondoke.

Inaelezwa baada ya mchongo huo, panga litahamia kwenye kikosi cha sasa ili kula vichwa ambavyo vimeshindwa kuonyesha maajabu Jangwani, licha ya matumaini makubwa wakati wanasajiliwa.

Mabosi wa Yanga wamechefukwa baada ya kuona msimu wa tatu timu yao inatoka kapa, pia wanashindwa kukata tiketi ya ushiriki wa mechi za kimataifa kwa kufungwa kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (AZFC) dhidi ya watani wao hao.