Simba yaendelea kuoga minoti

Muktasari:

Mabingwa watetezi na wawakilishi Tanzania katika mashindano ya kimataifa tutawakabidhi kitita hicho cha fedha kama zawadi kutoka kwetu tukiwa kama wadhamini wao kutokana na kutinga hatua hiyo ambayo haikufikiwa kwa muda mrefu

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wawakilishi wa nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, Simba wanatarajia kupokea kitita cha shilingi milion 50 kutoka SportPesa ikiwa ni kama motisha kutokana na kufanya vizuri Ligi Kuu na kimataifa.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema huo ni mwendelezo kwa timu zote zinazodhaminiwa na kampuni hiyo kupewa zawadi kutokana na mwenendo mzuri watakaokuwa wakionyesha.
Alisema Simba wamevuka hatua kubwa katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika wanastahili pongezi kama hiyo na kuweka wazi kuwa kama wataendelea kuvuka hatua nyingine hawatasita kuwapa tena fedha kama hiyo kwani ni hatua nyingine kubwa watakuwa wameingia.
"Simba inaenda vizuri ligi kuu pia na hatua ya wao kuweza kufanya vizuri katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, tunaomba kuendelea kuwaunga mkono kwa juhudi hizo wanazozionyesha tunatarajia kuwapa kiasi hicho cha fedha kama mwendelezo wa zawadi kwa timu zinavyofanya vizuri."
"Mabingwa watetezi na wawakilishi Tanzania katika mashindano ya kimataifa tutawakabidhi kitita hicho cha fedha kama zawadi kutoka kwetu tukiwa kama wadhamini wao kutokana na kutinga hatua hiyo ambayo haikufikiwa kwa muda mrefu," alisema.