Simba yaandika rekodi nyingine

Muktasari:

  • Omar Yassin wa Panama amekuwa mfungaji bora akiwa na mabao 9.
  • Clatous Chama ametajwa kuwa mchezaji bora wa ASFC hiyo kwa msimu huu.

HATIMAYE Simba imerejea kile ilichokifanya msimu wa mwaka 2016/17 baada ya kushinda mabao 2-1 mbele ya Mbao FC iliyokuwa imepanda Ligi Kuu msimu huo.

Simba imevuna tena ushindi wa namna hiyo kwa Namungo FC ambayo ni msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu na kutinga hadi fainali ya Kombel la Azam Sports Federation (ASFC) katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

Simba ndio ilikuwa ya kwanza kufumania nyavu za wapinzani baada ya bao la Luis Miquissone dakika ya 27 huku bao lao la pili likifungwa na John Bocco dakika ya 39.

Mabao hayo yaliwaweka Simba kifua mbele hadi dakika ya 56 Edward Manyama alipofunga bao moja kwa Namungo na kuwarejesha mchezoni.

Tangu michuano hiyo irejeshwe tena msimu wa mwaka 2015/16 kwa Yanga kuchukua ubingwa baada ya kuichapa Azam mabao 3-1 yaliyofungwa na Amissi Tambwe aliyetupia mawili kambani pamoja na Deus Kaseke huku goli la Azam likifungwa na Didier Kavumbagu.

Msimu uliofuata Simba ikaichapa Mbao FC kwa mabao 2-1 mchezo uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, msimu wa mwaka 2017/18 Mtibwa ikaichapa Singida United mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri beid, Arusha.

Msimu uliopita Azam nayo ikalinyakua kombe hilo baada ya ushindi wa bao 1-0 mbele ya Lipuli FC katika fainali iliyofanyika Lindi, kwenye Uwanja wa Ilulu.

Miquissone alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa fainali na kujinyakulia Sh 500,000.

Namungo FC na Simba kabla mchezo huo zilikuwa zimekutana mara tatu, mchezo wa kwanza zilikutana Julai 8 mwaka Juzi na kutoka suluhu katika mchezo wa kirafiki wakati Namungo FC ikiuzindua Uwanja wao wa Majaliwa.

Mchezo wa pili zilikutana Januari 29 mwaka huu na Simba kuibuka na ushindai wa mabao 3-2 Uwanja wa Mkapa na katika mchezo wa marudiano Julai 8 mwaka zikitoka suluhu.

Wachezaji walioanza kwa upande wa Simba, langoni alikaa Aishi Manula, huku safu ya ulinzi akiwa, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Kennedy Juma na Pascal Wawa.

Viungo ameanza, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Gerson Fraga, na safu ya ushambuliaji akiwa John Bocco, Clatous Chama na Francis Kahata / Hassan Dillunga.

Kwa upande wa Namungo FC, Nourdine Barola, Rogers Gabriel, Edward Manyama, Steven Duah, Karlos Protas, Hamis Khalifa, Hashim Manyanya / Frank Mkumbo, Daniel Joram, Bigirimana Blaise, Lucas Kikoti, Abeid Athuman.