HISIA ZANGU : Simba ya zamani katika akili mbili mpya za kisasa

Muktasari:

  • Kuelekea katika mechi hiyo Simba waliachana na upuuzi fulani hivi ambao umezoeleka katika soka letu. Hawakwenda nje ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo. Walibakia hapa hapa Dar es salaam wakaenda zao uwanjani.

WALINIKOSHA Simba kwa jambo moja wakati tukielekea kuufunga mwaka jana. Oktoba walicheza na Yanga katika Uwanja wa Taifa. Itakumbukwa kama mechi ya Beno Kakolanya. Alikuwa katika ubora wake.

Kuelekea katika mechi hiyo Simba waliachana na upuuzi fulani hivi ambao umezoeleka katika soka letu. Hawakwenda nje ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo. Walibakia hapa hapa Dar es salaam wakaenda zao uwanjani.

Walipofika uwanjani walicheza mpira mkubwa. Walimiliki mpira kwa asilimia 90. Kwa muda mrefu sijawahi kuona pambano la upande mmoja kati ya Simba na Yanga kama lile. Nikajiuliza, waliathirika nini kwa kutokwenda Zanzibar au Morogoro?

Hii tabia ya Simba au Yanga kwenda Morogoro au Zanzibar imekuwa mazoea tangu enzi na enzi. Mwisho wa siku sioni kama kuna kitu chochote kinachobadilika katika mechi kupitia safari hii ya usumbufu kwa wachezaji.

Wakati mwingine inaonekana kuwa ni upotevu wa muda na pesa. Wakati mwingine huwafanya wachezaji wajikute katika presha kubwa na kudhani ni mechi tofauti sana uwanjani. Wengine wanashindwa kwa sababu ya hofu tu na kukosa usingizi kutokana na mikutano mingi na waganga wa kienyeji inayoendelea katika hoteli zao.

Zamani TFF ikiwa inaitwa FAT ilikuwa inasimamisha mechi za Simba na Yanga kwa wiki mbili kwa ajili ya kupisha maandalizi ya mechi hiyo. Ujinga ulioje!. Wakati huo huo Manchester United na Manchester City zinaweza kucheza Jumamosi huku zikiwa zimetoka kucheza mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa siku ya Jumatano.

Shukrani kwa Simba ambayo imeanza kung’amua kuwa hakuna umuhimu wowote wa kupeleka timu Morogoro au Zanzibar kama una kikosi kizuri. Bahati mbaya Simba ilikosa mabao mengi katika mechi ya Yanga. Je, ilitokana na timu kutokwenda Zanzibar? Siamini katika hilo. Ninachojua ni kwamba watu wa kamati wa ufundi wanaweza kuleta kisingizio hiki.

Kinachoshangaza zaidi kwa timu zetu wiki moja kabla hawajacheza mechi ngumu ya kimataifa kama vile dhidi ya Al Ahly huwa wanabakia hapa hapa Dar es Salaam wakifanya maandalizi. Wakicheza dhidi ya watani katika pambano la kukamilisha ratiba ya ligi huwa wanakwenda Pemba.

Achana na hilo. Mwaka huu Simba imeanza kwa kunikosha kuelekea katika pambano lake la kimataifa dhidi ya JS Soura Jumamosi. Simba imeamua kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi pale Zanzibar. Awali nilidhani ingepeleka kikosi B au ingejitoa katika michuano.

Kuelekea katika mechi za kimataifa timu zetu inabidi ziendelee kucheza ligi kwa ajili ya kujiweka fiti. Naelewa hoja ya kujitoa kucheza mechi kadhaa za nje ya Dar es Salaam kwa sababu za ubovu wa viwanja vya mikoani pamoja na matatizo ya usafiri wa muda mrefu.

Wachezaji wanapokusanyika na kufanya maandalizi ya mazoezi kwa wiki mbili hakuna wanachojipima. Mazoezi ni tofauti na mechi. Mechi huwa inakuwa na presha tofauti na ile ya mazoezi. Ni vema kucheza mechi wakati wa kuelekea katika maandalizi kuliko kufanya mazoezi peke yake.

Kuna watu wanadai mechi za kuelekea katika mechi kubwa zinaweza kuleta majeruhi kama ilivyotokea kwa Erasto Nyoni juzi Jumapili. Ukweli ni mchezaji anaweza kuumia popote. Mungu ndiye ambaye anapanga mchezaji kuumia. Mchezaji anaweza kuumia mazoezini, anaweza kuumia chumbani kwake, anaweza kuumia wakati akipasha misuli yake moto dakika chache kabla ya mechi. Imetokea mara nyingi.

Halafu kuna wale ambao wanakata tamaa kwa sababu timu inaweza kucheza vibaya au kubanwa mbavu siku chache kabla ya mechi za kimataifa. Kwa mfano juzi ambavyo Simba ilibanwa mbavu na KMKM. Ukweli mechi dhidi ya KMKM na ile dhidi ya JS Soura ni vitu viwili tofauti.

Wachezaji hucheza mechi kutokana na presha ya mechi. Mechi ya JS Soura wachezaji wataipokea kwa umuhimu mkubwa kuliko mechi ya KMKM.

Majukwaa pia yatawahimiza kufanya kazi tofauti na ile ambayo waliifanya juzi katika Uwanja wa Amani. Hivi ndivyo mpira ulivyo. Hotuba ya kocha na viongozi kuelekea mechi ya JS Soura zitakuwa tofauti na maneno machache ambayo wachezaji waliambiwa kuelekea katika mechi ya Zanzibar juzi. Wachezaji wataipokea mechi hii ya JS Soura kwa kuangalia pia manufaa yao binafsi wanavyoweza kupata wakifanya vema.

Wakati wa kubadili baadhi ya tamaduni umefika. Tusiishi kwa kukariri sana baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanafanywa na watu wa zamani. Leo kuna viongozi wenye damu changa ambao wanafuatilia mpira wa Ulaya unavyochezwa kila kukicha na wanapaswa kutuonyesha wanaweza kuiga kwa mafanikio kinachoendelea nchi hizo. Haya mawili kutoka kwa Simba yamenikosha. Kutokimbilia Zanzibar kujificha katika mechi dhidi ya Yanga na bado wakaonyesha uwezo mkubwa uwanjani. Na pili hili la kutumia wachezaji wazoefu katika mechi za Mapinduzi wakati wamebakiza siku chache kucheza dhidi ya JS Soura. Kuna kitu cha kujifunza hapo.