Simba ya moto VPL

Muktasari:

Simba imekuwa katika kiwango bora tangu ilipotoka sare na Mtibwa Sugar ya 1-1.

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza msimu huu kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck amewaanzsiha washambuliaji wawili kwenye kikosi cha kwanza katika mechi ya JKT Tanzania, Meddie Kagere na Chriss Mugalu.

Sven alicheza karata iliyompa majibu mapema kwani ndani ya dakika sita za kwanza, washambuliaji hao walishafunga.

Kikosi hiko cha Simba katika mechi tano za awali kimeshinda nne, sare moja, hakijafungwa, huku kikiwa na mabao 14 na kufungwa mawili katika pointi 13 ilizokusanya.

Mabingwa hao watetezi wa ligi wamefanya usajili wa wachezaji saba msimu huu, kati ya hao, huku Joash Onyango akiwa mpya pekee mwenye uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza.

Larry Bwalya, Bernard Morrison na Mugalu wote wakiwa na ubora, lakini bado wanaingia na kutoka katika kikosi cha kwanza.

Aina hiyo ya usajili ambao wameufanya Simba msimu huu ni nadra kuona mchezaji kama Bwalya, Morrison na Mugalu wanawekwa nje katika timu nyingine nchini.

Sehemu nyingine ambayo imeimarika kwa Simba ni uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja kama ambavyo amekuwa akionyesha Cletous Chama, Bwalya, Luis Miquissone pamoja na wengine.

Sven amekuwa na uwanja mpana wa kuchagua wachezaji watakaoanza kikosi cha kwanza na ambao watakuwa benchi kama mbadala wa wenzao.

Simba msimu huu wanaweza kuwakosa John Bocco, Francis Kahata, Ibrahim Ajibu, ambaye licha ya uwezo wake mkubwa alionao anaonekana kama mchezaji wa kawaida.

Uwezo wa Ajibu, Hassan Dilunga, Said Ndemla na wengineo, kwenye timu nyingine ni wachezaji wa kutegemewa kikosi cha kwanza.

Eneo lingine ambalo Simba wameimarika msimu huu mbali ya Sven, kupenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1, anaweza kuwa na machaguo ya mifumo mingine kama ambavyo alifanya juzi dhidi ya JKT Tanzani.

Washambuliaji wanne wa Simba, Bocco, Kagere, Mugalu na Charles Ilanfia wameongeza makali na ushindani katika kikosi msimu huu kutokana na uwezo wao wa kufunga.

Ubora wa nyota hao umeimarisha kikosi cha Simba, kwani Kagere katika mechi tano za ligi amefunga mabao manne, wakati Mugalo akifunga matano katika mechi tano.

Wakati Bocco katika mechi sita za msimu huu alizocheza amefunga mabao mawili kama ilivyokuwa kwa Ilanfia aliyefunga mawili katika michezo miwili.

Sven alisema miongoni mwa maeneo ambayo timu yake imeimarika ni ushindani kutokana na kila mchezaji kuonyesha uwezo.

“Kuna wakati hadi naumiza kichwa kuchagua nyota 18 wa kuwakilisha wenzao, kwani wote kikosini ni bora kutokana na viwango wanavyoonyesha,” alisema.

Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Etienne Ndayiragije anasema alipata nafasi ya kwenda kushuhudia mazoezi ya Simba na kuwaona Mugalu na Kagere wakifunga mabao ambayo yamekuja kujitokeza tena katika mechi na JKT.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema uimara wa kwanza ambao timu yake ya zamani umeonekana ni kwa kipa Aishi Manula, ambaye msimu uliopita alikuwa na makosa mengi.

“Tangu miaka 25, iliyopita Simba lazima iwe na kipa mwenye uwezo, beki wa kati mwenye akili kama ambavyo safu ya kiungo iwe na watu wa kuzalisha mabao ambayo itakwenda kuwakuta mastraika wenye uwezo wa kufunga,” alisema beki huyo wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars.