Simba ya Mbelgiji haiachi kitu

KOCHA wa Simba Mbeligiji Patrick Aussems

KOCHA wa Simba Mbeligiji Patrick Aussems ameanika hadharani kikosi chake kipya, lakini akisisitiza watakaopata nafasi ndani ya kikosi chake cha kwanza lazima jasho liwatoke kwa kuwa anataka kufanya kweli kila michuano watakayoshiriki.

Patrick aliyeambatana na kikosi hicho mjini Lindi, alisema anataka kuwa na kikosi cha wachezaji 18 walio fiti kwa kushambulia haraka huku wakicheza soka la kupasiana muda wote na ikitokea wamepoteza mpira kila mchezaji anatakiwa kuwa na jukumu la kukaba haraka pia.

Alisema awali alikuwa anataka kuwaona wachezaji wote ili kufahamu uwezo wake jambo ambalo ameshafanikiwa tayari na kinachofuata sasa ni kutafuta wale ambao watakuwa bora kwa kutimiza majukumu yao kila anapowapa nafasi.

Aussems alisema katika hizi mechi tatu alizocheza awali na mbili watakazocheza kwenye ziara yao mkoani Lindi na Arusha atawatumia pia wale wachezaji ambao hawakupata nafasi ili ajiweke tayari kwa mechi ya Ngao ya Hisani wikiendi ijayo.

“Naendelea vizuri kwa kushirikiana na wasaidizi wangu na kabla ya kuanza kwa Ligi nitakuwa nimeshapata kikosi kamili ambacho kitakwenda kufanya yale ya msingi ambayo nawapatia tukiwa mazoezini na kuvuna pointi tatu katika kila mechi.”

Aussems alisema anataka kikosi chake kifanye vema katika kila shindano wakianza na Ngao ya Jamii kabla ya kugeukia Ligi Kuu, Kombe la FA na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Hapa Simba wachezaji wote wapo katika viwango bora jambo linalonipa matuamini tutafanikiwa kwa kila tunalolipanga kwa msimu ujao,” alisema.

“Kiukweli nina matumaini makubwa na timu yangu inakwenda kufanya vizuri msimu huu katika mashindano yote na nimekuwa nikiwapa kila mbinu wachezaji wangu ili kulitimiza hilo kwani ndio kiu yetu,” alisema.

BOCCO, KAPOMBE BADO

Nahodha wa Simba John Bocco alishindwa kucheza mechi ya Simba Day katikati ya wiki hii dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana kwa kuwa ni majeruhi tangu akiwa kambini Uturuki, lakini siku 11 za kujiuguza anaelekea vyema, lakini bado hajaanza kuchangamana na wenzake.

Hali hiyo ipo pia kwa Shomary Kapombe aliyekuwa yupo fiti mpaka katika mechi na Kotoko kabla ya kuumia mguu wa kulia dakika ya 16 wakati mechi hiyo ikiendelea na alitolewa na nafasi yake alichukua Mghana Nicholas Gyan.

“Bocco hataweza kuwa na sisi katika safari ya Lindi nimemweleza aendelee na mazoezi yake mapesi na atakuja kuungana na sisi tukiwa Arusha lakini hata sitamtumia pia mpaka nitakapolizika nae,” alisema.

“Kapombe alikosekana katika mazoezi ya leo (jana) asubuhi kwani alikwenda hospitali ili kupata matibabu zaidi nadhani nitapata taarifa kamili kutoka kwa daktari,” alisema Aussems.

“Bocco anaendelea vizuri anafanya mazoezi mepesi lakini Kapombe nae hajapata jeraha kubwa nadhani atachukua kama siku tatu kuwa nje ya uwanja,” alisema daktari wa Simba, Yassin Gembe.