Simba ya MO bado hapa tu

Muktasari:

  • Lakini kuna mengine ambayo aliyaahidi bado yanasubiriwa kwa hamu na kuona yanatekelezwa na Mwanaspoti linakuletea mambo sita yaliyoahidiwa na MO ambayo bado yanasuasua na ni wazi huenda ikawa ni mtihani kama atashindwa kufanyikisha kwa haraka kuanzia sasa.

NI miezi 10 sasa tangu mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Klabu ya Simba yalipopitishwa rasmi Mei mwaka jana ambapo pamoja na mambo mengine, Bilionea Mohammed ‘Mo’ Dewji alitangazwa kuwa mwekezaji mkuu ndani ya klabu hiyo.

Baada ya kutangazwa kuwa mwekezaji mkuu, bilionea huyo alitangaza baadhi ya mambo ambayo angeanza nayo kama kipaumbele na kuwafanya Wana Msimbazi kuwa na hamu ya kuona yakitekelezwa kwa haraka.

Moja ni kutaka kuiona Simba ikifika mbali katika michuano ya Afrika na kweli mpaka sasa timu ipo hatua chache kabla ya kutinga robo fainali kutoka Kundi D, katika hilo, Mo Dewji na vijana wake wanastahili pongezi za dhati.

Lakini kuna mengine ambayo aliyaahidi bado yanasubiriwa kwa hamu na kuona yanatekelezwa na Mwanaspoti linakuletea mambo sita yaliyoahidiwa na MO ambayo bado yanasuasua na ni wazi huenda ikawa ni mtihani kama atashindwa kufanyikisha kwa haraka kuanzia sasa.

UJENZI WA OFISI MPYA

Licha ya klabu hiyo kupata mwekezaji ambaye ni mfanyabiashara mkubwa barani Afrika, Simba imeshindwa kujiendesha kisasa kama ilivyo kwa klabu kubwa barani Afrika ambazo zimejipanga kuanzia viwanja hadi miundombinu ya kimichezo, Simba haina ofisi za kueleweka.

Simba ina jengo kubwa katikati ya jiji ambalo kiuwekezaji hata kiusimamizi lingeweza kuwalipa hata wachezaji mishahara lakini kutokana na usimamizi mbovu limekosa msaada kutokana na kushindwa kutumika ipasavyo kama kitega uchumi.

Pamoja na kuwa na wapangaji wengi wanaoendesha biashara zao lakini, halijawa na manufaa yoyote kwa klabu. Pia, ilitegemewa kama jengo hilo lingetumika kama ofisi za viongozi lakini ni tofauti, hivyo kuna jambo la kufanya kwa Mo Dewji kuhakikisha anajenga ofisi ya maana ambao itawakutanisha viongozi wote tofauti na sasa kila mmoja anafanya kazi anapojua yeye.

Achana na viongozi wengine wa chini hata kwa upande wake mwenyewe amekuwa akifanyia mambo yake ya kibiashara na mpira katika ofisi yake ambayo pia amekuwa akiitumia kuzungumza na wanahabari jambo ambalo sio zuri kwa maendeleo ya kimpira kama anataka kufikia mafanikio makubwa kama ya TP Mazembe.

UJENZI WA UWANJA

Kilikuwa ndio kipaumbele chake cha kwanza kabisa alivyokuwa anaomba udhamini katika klabu ya Simba na aliweka wazi kuwa hadi Februari mwaka huu atakuwa amekamilisha uwanja wa mazoezi.

“Mwaka wa kwanza kwa kushirikiana na wanachama tutakuwa na kiwanja cha nyasi asilia na kiwanja cha nyasi bandia tutatumia kwa mazoezi kwa kadiri ya mahitaji ya mechi tutakazoenda kucheza pia, tutajenga hosteli vyumba 35 wataishi wachezaji 30 na stafu,” anasema.

Lakini hadi sasa Simba ameshindwa kufikia malengo hayo, kama alivyoahidi japo mambo ya kuandaa uwanja huo yalianza huku kikwazo kikubwa kikiwa ni nyasi bandia ambazo zimekwama bandarini zikiwa kama ushahidi wa kesi inayowakabiri viongozi wa klabu hiyo wanaoshikiliwa.

AJIRA MPYA

Tangu wameingia katika mfumo mpya wa mabadiliko uongozi wa Simba chini ya Mwekezaji wao Mo Dewji, ulitangaza uboreshwaji wa idara mbalimbali ndani ya klabu na kuimarisha benchi la ufundi.

Ni moja tu ambalo limeshafanyika hadi sasa ambapo wamefanikiwa kumsajili kocha msaidizi kwaajili ya kusaidiana na Kocha Mkuu, Patrick Aussems wakati kulikuwa na nafasi mbili ambazo ziliwekwa wazi kuwa ni lazima zitafutiwe ufumbuzi ambazo ni Mkurugenzi wa Ufundi na Mkurugenzi wa Wanachama, mpaka sasa hayo hayajafanyiwa kazi.

USAJILI WA MAPRO

MO alisema ukitaka kuwa na wachezaji bora lazima utumie pesa. Nia yake ilikuwa kiwango cha chini cha usajili kiwe chini ya bilioni moja kwa mujibu wake.

Lakini hivi karibuni amekiri usajili walioufanya haukukidhi kushindana na klabu kubwa wanazokutana nazo katika Mashindano ya Afrika.

Kununua wachezaji bora ambao watawezesha kufikia malengo ya kuwania mataji bora barani Afrika alisema wanamtaji mkubwa wa mashabiki na amegundua Simba ndio brand kubwa nchini kutokana na kuwa taasisi inayotajwa sana kutokana na kuwa na wafuasi wengi, hivyo kutumia vyema mtaji huo kwa kuwekeza.

WADHAMINI WAPYA

Licha ya kuwekeza kwake kiasi kikubwa cha fedha alisema anatamani kuona wawekezaji wengine wanaingia hapo ili waweze kuiendesha klabu ikiwa na fedha kubwa ambayo inaweza kuwazidi wapinzani wake na kuanza kushindana nao.

Kitu hicho hadi sasa hakijafanikishwa ndani ya uwekezaji wake na amekiri kuwa ndio moja ya changamoto ambayo inawakwamisha wao kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ambayo hadi sasa wao ndio wawakilishi pekee waliobaki.

KLABU KUJIENDESHA KIBIASHARA

Ni miongoni mwa vipaumbele vyake kabla na baada ya kukabidhiwa timu. Katika mipango yake ilikuwa ni kuhakikisha timu inajiendesha kibiashara na kuingia katika ushindani kwa timu kubwa nje ya Tanzania na sio ndani pekee kwa namna moja ameshgindwa kufanya hivyo na kuahidi kuendelea na mapambano.

Mwekezaji huyo kwa kinywa chake amekiri: “Tangu tulipofanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu mpaka sasa ni hasara na hili katika biashara ni jambo la kawaida ingawa tunajua faida itakuja baadaye.

“Hata faida ikianza kupatikana, kinachofuata ni kuendelea kuwekeza fedha kwenye klabu kwa kuwa lengo si kutengeneza fedha, bali kuifanya klabu iwe na msingi endelevu wa kujiendesha, tukija kuondoka, Simba iweze kujisimamia,” Mo Dewji alinukuliwa wiki chache zilizopita.