Simba wasoma albadiri

Muktasari:

  • Hadi sasa bado hali ya hewa haijatulia baada ya kutekwa kwa Bilionea, Mohammed Dewji (43) lililotokea juzi Alhamisi alfajiri Dar es Salaam katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Osterbay.

WAKATI taharuki ikiwa bado imetawala nchi nzima kutokana na kutoweka kwa bilionea na mwanachama mashuhuri wa Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji aliyetekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya juzi Alhamis, Wazee na wanachama wa klabu hiyo wameangusha dua nzito klabu kwao jana Ijumaa kwa nia ya kumuomba Mungu amsaidia bilionea huyo.

Huku katika makao makuu ya klabu hiyo wakiangusha dua hiyo, mpaka sasa bado kumekuwa na ukimya juu ya mahali alipo bilionea huyo na mtu aliyetarajiwa kuwa mwekezaji wa Simba katika mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo ya Msimbazi.

Mbali na kutofahamika mahali alipo mpaka sasa, bado wanachama na mashabiki wa Simba sambamba na wadau wengine wa michezo wamekuwa wakitoa maoni yao na wengi wakimuombea aweze kupatikana akiwa hai.

HALI ILIVYO SASA

Tangu juzi baada ya tukio la MO Dewji kutekwa na watu wasiojulikana ikielezwa ni wazungu wawili katika hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam alipoenda kwa ajili ya kufanya mazoezi bado giza nene limetanda mpaka sasa.

Sio jeshi la polisi wala familia ya bilionea huyo waliokuwa tayari kusema kinachoendelea, lakini ikielezwa upepelezi unaendelewa kufanywa ikiwemo kuhojiwa kwa watu mbalimbali ili kupata picha halisi ya kilichompata mfanyabiashara huyo maarufu Afrika.

Mwanaspoti iliyoweka kambi Kituo Kikuu cha Polisi, ilishindwa kupata chochote kipya zaidi ya kuelezwa watu 12 wamekamatwa, wengi wakiwamo walinzi na watumishi wa hoteli hiyo, huku maofisa wa juu wa hoteli hiyo nao wakiendelea kuhojiwa na polisi.

Gari la MO bado lipo eneo lile lile lililoachwa juzi, lakini ulinzi ukiongezwa maradufu kuliko ilivyokuwa juzi muda mchache baada ya tukio hilo, huku eneo hilo likiwa limetulia na kuonekana maafisa usalama wakipita hapa na pale sambamba na wanahabari waliokuwa wamepiga kambi hapo ili kujua chochote kipya.

NYUMBANI kwake

Nyumbani kwa bilionea huyo Mtaa wa Laibon, Oysterbay nako kumezizima kwani wanafamilia walikuwa bado wakitafakari kilichomkuta ndugu yao, huku baba yake

Gulam Dewji akikataa kuzungumza lolote kwa madai kuwa, suala hilo la kwa sasa lipo mikononi wa vyombo vya dola na asingependa kusema lolote.

Hata msemaji wa familia hiyo naye imeelezwa amezuiwa kuzungumza, ingawa ndugu wengine wamekuwa wakiingia na kutoka katika nyumba hiyo kwa ajili ya kufarijiana huku kinamama baadhi ya wakionekana kulia kwa simanzi.

ULINZI WA KUTOSHA

Katika eneo la Yatch Club ambako nako maafisa wa Polisi wamekuwa wakifuatilia, Mwanaspoti imekutana na ulinzi mkali na Meneja wa eneo hilo, Brian Fernandez alisema ulinzi umekuwa maradufu na hakuna aliyeruhusu kutoa boti katika eneo hilo.

Fernandez anakiri kuwa, Mo ni mwanachama wa klabu hiyo ya watu mashuhuri, lakini hakumbuki ni lini bilionea huyo alifika hapo, huku akisisitiza maafisa wa Polisi walikuwa ndani wakikagua kamera za usalama (CCTV) ili kuambulia chochote cha kuwasaidia katika shughuli zao.

WAZEE WAANGUSHA DUA

Makao makuu ya klabu hiyo mchana wa jana kulikuwa na tukio moja la aina yake lililofanywa na Wazee sambamba na wanachama wa klabu hiyo kwa kuangusha dua nzito ili kumuombea Mo Dewji aweze kuwa salama huko alipo na kupatikana akiwa hai ili mambo yaendelee Msimbazi.

Dua hiyo iliyoendeshwa na masheikh maalum huku ikihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Simba wa sasa na wa zamani wa klabu hiyo na ilianza saa 7:20 mchana mara baada ya swala ya Ijumaa ambapo hata hivyo wanachama na mashabiki wa klabu hiyo walianza kumiminika klabu hapo tangu saa 7:00.

Kwa zaidi ya sasa 1 dua hiyo ilingurumishwa baada ya kufunguliwa na Kaimu Katibu Mkuu, Hamis Kissiwa, huku akiongozwa na Mwenyekiti wa zamani, Hassan Dalali aliyeambatana na masheikh hao.

MBUZI WACHINJWA

Kabla ya kusomwa kwa dua hiyo, mbuzi wawili mmoja mweupe mwenye madoa meusi na mwingine wa rangi ya krimu, waliingizwa klabuni hapo na kuchinjwa, japo Mwanaspoti na waandishi wengi walizuiwa wasishuhudie wakati wa tukio hilo.

Dalali aliyekuwa sambamba na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tulliy na wengine waliohudhuria walifafanua dua hiyo kwa kudai ni maalum kwa kumuombea Mo huko alipo sambamba na kuomba Mungu amjalie arudi salama.

MANARA ANASWA

Katika hatua nyingine inadaiwa kuwa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alikamatwa na kushikiliwa na Polisi kabla ya kuachiwa na jana kuitwa tena kwa ajili ya mahojiano, ingawa hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa tayari kuthibitisha.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alithibitisha juu ya kushikiliwa na kuhojiwa kwa Manara kutokana na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii akidai ametumwa na familia jambo ambalo sio kweli.

MAMBO YASIMAMA

Kitendo cha kutekwa kwa Mo Dewji kumestua watu wengi ndani na nje ya nchi, hiyo ni kutokana na umaarufu wake ikiwemo utajiri alionao, lakini viongozi na wanachama wa Simba wameshtushwa zaidi kwani kuna mambo kwao yatakwama.

Inaelezwa mambo mengi ndani ya Simba yamesimama kwa sasa na kuwapa taharuki zaidi, ingawa ishu ya ujenzi wa uwanja wao wa Bunju inaendelea kwa vile tayari MO alishamalizana na mkandarasi na vifaa vya kutosha kuwepo kwa ujenzi huo.

Mmoja wa viongozi wa Simba, aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alisema hali ya Simba kwa sasa ni tete kwa vile hajui wataishije bila ya Mo, lakini kilichomkuta bilionea huyo kimewavuruga kiakili kiasi cha kushindwa hata kufanya mambo yao ya kawaida.

Mo Dewji ndiye mfadhili na mdhamini wa klabu hiyo kupitia kinywaji chake cha Mo Energy huku akiwa mzabuni pekee aliyepita katika mchakato wa uwekezeji ndani ya Klabu hiyo ambapo itaondoka kwenye mfumo wa wanachama na kuwa kampuni.

Mo alitangaza kuwekeza Sh20 bilioni kwa asilimia 49 na michakato ya kuhama kutoka mfumo wa zamani imeanza kwa kubadilisha katiba na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao Novemba 4 wa kuwapata wajumbe saba watakaoiwakilisha klabu kwenye Bodi ya Wakurugenzi hapo baadaye.

UWANJA WA BUNJU

Hivi karibuni, Mo alianza pia kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa uwanja wa Bunju na ujenzi huo umeanza kwa upande wa uwanja wa mazoezi unaogharimu Sh600 milioni kukamilika kwake.

Ujenzi wa uwanja huo umeendelea kama kawaida kwa sababu tayari kila kitu kilikuwa kimenunuliwa na Eng Danny anayejenga uwanja huo kupitia Kampuni ya Masasi Constraction Company Limited.

“Tuliingia mkataba, hivyo ni lazima kazi ziendelee kama kawaida, kila kitu kilinunuliwa na wiki ijayo tutaingia hatua nyingine, kikubwa tuendelee kumwombea Mo huko aliko awe salama na arudishwe salama,” alisema Eng Danny.

ISHU YA KOCHA MSAIDIZI

Imeelezwa kutokana na tukio hilo kubwa lililotikisa nchi, mambo mbalimbali ndani ya Simba kwa sasa yamesimamishwa likiwemo suala la kocha msaidizi ambaye alianza kujadiliwa katika kikoa chao kilichofanyika mapema wiki hii dhidi ya viongozi wa klabu na Mo.

Kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems aliwaomba viongozi kumtafutia msaidizi wake mzawa na tayari kuna majina matatu ambayo yamependekezwa likiwemo jina la Kocha wa Mbao, Amri Said.

“Kwa sasa akili na mawazo yote yameelekezwa kwenye suala hilo ingawa lipo chini ya Polisi, ila mambo mengi ndani ya klabu yamesimama, hatuwezi kufanya lolote hadi hapo baadaye kidogo tukikutana na kujadili, hata mpango wa kocha msaidizi hauwezi kujadiliwa kipindi hiki,” alisema kiongozi huyo.

UCHAGUZI MKUU

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema Kamati ya Uchaguzi ilipanga kukutana juzi Jumatano kutangaza majina ya wagombea wote waliopita kwenye uchaguzi huo, lakini baada ya tukio hilo kila kitu kilivurugika huku baadhi ya wajumbe wakiwa na wasiwasi uchaguzi huo kusogezwa mbele.

MISHAHARA NA POSHO

Bajeti ya Simba kwa mwezi ni zaidi ya Sh230 milioni kwa mwezi na hutumika kulipa wataalamu wa benchi la ufundi, mishahara na posho kwa wachezaji pamoja na shughuli zingine za klabu.

Kutokana na tukio hilo kama litachukua muda mrefu basi uongozi wa Simba utapaswa kuanza kupunguza matumizi ili kuendena na hali halisi ya uchumi wa klabu.

Matumizi watakayopaswa kupunguza ni kutumia usafiri wa anga wanapokwenda kucheza mechi za mikoani hasa mikoa ya mbali kama Kanda ya Ziwa na Mbeya, posho, kuongeza wataalamu wengine wa benchi la ufundi na walikuwa kwenye mchakato wa kuajiri daktari kutoka India.

MIKOANI

WASHTUSHWA

Jijini Mbeya wadau wa soka wametoa maoni yao na kusema kitendo cha kutekwa kwa Mo Dewji kimewaogofya na ni kitu cha hatari na Watanzania wanahitaji kushikamana katika kipindi hiki kigumu.

Mwenyekiti wa mashabiki wa Simba Mkoa wa Mbeya, John Bondo alisema; “Inauma sana na kitu ambacho hatukuwahi tegemea kama lingetokea hili. Hapa kwa sasa Watanzania na mashabiki wa Simba tunahitaji kuwa na mshikamano, umoja na kila mmoja wetu azidi kuomba kwa kila aina ya dua kuona kiongozi wetu huko aliko awe salama wakati vyombo vyetu vya usalama vikiendelea na kazi yake,” alisema Bondo.

Naye Katibu Mkuu wa Prisons, Havintishi Abdallah alisema tukio hilo limeitikisa nchi na mataifa mengine na ni jambo la kuogofya na kusikitisha.

“Aisee hii si kwa wapenzi wa soka tu ni kwa Watanzania wote. Inatupa mashaka mno. Yule ni mtu muhimu sana Tanzania na Afrika nzima. Sisi Prisons, tunaiomba sana Serikali kupitia vyombo vyake vya dola ifanye kazi yake kuhakikisha anapatikana akiwa hai na salama”.

Huko Arusha nako kutekwa kwa Mo Dewji kumezua tafrani kwa wadau wa soka hasa wa klabu za Simba na Yanga na tawi la Arusha wameamua kufunguka ya moyoni.

“Tumepokea taarifa hizo si kwa masikitiko pekee bali kwa mshtuko pia maana ingawa MO (Dewji) ni shabiki na mlezi wa klabu ya Simba lakini ni moja wa viongozi matajiri Tanzania na Afrika nzima lakini huwa hajivuni bali ni mnyenyekevu muda wote hivyo hili tukio si la watu wa simba pekee bali hata Yanga na wadau wote wa soka na maendeleo ya Taifa,” alisema Athumani Kihamia ambae ni mjumbe wa kamati ya mashindano ya Yanga. Kihamia ambaye pia ni Mjumbe Kamati ya Uwekezaji TFF, amewaomba wanachama na mashabiki pia wadau wa michezo nchini kuungana na vyombo vya vya ulinzi katika kuhakikisha mwekezaji huyo wa klabu ya Simba anapatikana badala ya kuzusha taarifa za tukio hilo na kusambaza kwa mitandao au kuponda juhudi zinazofanyika na vyombo vya ulinzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Yanga, Arusha, Mhina Kahoya alisema matukio ya kutekana sio ya kibinadamu na wao kama Tawi la Yanga Arusha wanalilaani kwani mbali na MO (Dewji) kuwa mwekezaji na mlezi wa Simba lakini amekuwa akitoa changamoto kubwa pia kwao katika kupambania maendeleo ya soka Tanzania.

“Tumesikitika sana na tunalaani tukio hilo ni kumwombea kwa Mungu asidhurike huko alipo na apatikane akiwa hai maana hatujui huko alipo anapata mateso gani na yuko katika hali gani, hivyo tuzidi kuungana na kuzidisha maombi baya lisimpate.

Nao Wanachama wa Simba Tawi la Arusha wameitana katika ofisi zao zilizoko mjini kati Mtaa wa bondeni na kufanya sala maalumu ya kumwombea mwekezaji wao kila mmoja kwa imani yake.

“Ni tukio ambalo limezua taharuki na simanzi na masikitiko kwa familia yake na jamii kwa jumla na limeshtua wengi siyo sisi pekee, bali Afrika nzima wanaomfahamu, hivyo katika kuamini Mungu anaweza zaidi ya mwanadamu tumeitana leo tukafanya ibada maalumu asubuhi kumwombea asidhurike na apatikane akiwa hai,” alisema Katibu wa Simba tawi la Arusha, Thabit Ustaadh.

BAYI LIMEMCHOMA

Licha ya Polisi kueleza kuwashikilia baadhi ya watu kutokana na tukio hilo, wanariadha maarufu nchini wametoa tahadhari kwa Watanzania kutokana na tukio hilo wakiwasisitiza kuchukua tahadhari mapema.

Nyota wa zamani wa riadha na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema ni wakati wa kujihadhari kwa kuwa maadui ni wengi na hawatoki mbali.

“Sitaki kulizungumzia sana suala hilo kwani liko chini ya Polisi na matumaini ya kuhakikisha Mo anapatikana yapo, lakini hili linatoa funzo gani kwetu? Tujihadhari na maadui kwa kuwa wanatoka mule mule kwa marafiki,” alisema Bayi.

Alisema mtu asijekufahamu hawezi tu kuibuka na kukufanyia tukio la ajabu, lazima anatoka miongoni mwa watu wanaokufahamu vyema, hivyo ili kuwa salama ni lazima kuchukua tahadhari mapema,” alisema Bayi ambaye pia ni mmiliki wa shule za Filbert Bayi.

Nyota wa zamani wa Olimpiki na kocha wa timu ya taifa ya riadha ya Brunei, Sulemain Nyambui alisema tukio hilo ni funzo kwa kila mmoja, licha ya kuwashauri wanariadha hususan wale waliofikia viwango vya kupata fedha nyingi kwenye mbio kuwa waangalifu zaidi.

“Hiyo ni hali hatarishi, lakini naamini kwa uwezo wa Mungu na jitihada za jeshi la Polisi, ndugu yetu huyo atapatikana na waliofanya tukio hilo watachukuliwa hatua, lakini ni wakati sasa wa kuwa waangalifu.

“Hata wanariadha wale wanaopata fedha nyingi kwenye mbio, wahakikishe wanafanya mazoezi sio peke yao, wajifue wawili au zaidi, kwani watekaji wanahitaji vitu vingi, wengine wanataka fedha, hivyo ni wakati wa kuchukua tahadhari mapema,” alisema Nyambui moja kwa moja kutoka Brunei.

Nyota wa mbio ndefu nchini, Alphonce Simbu alisema tukio hilo limeshtua kweli kweli na limeibua maswali mengi bila majibu, japo naye ameungana na watangulizi wake kumwombea Mo apatikane na kuungana tena na familia yake.

“Hatukuwahi kufikiria mambo kama hayo, hivi kwa mtu kama Mo kutekwa, inabidi kujiuliza mara mbili mbili vipi kuhusu wengine? Cha msingi ni kuchukua tahadhari na tuendelee kumwombea apatikane salama,” alisema Simbu.

BINSLUM AFUNGUKA

Mmoja wa wafadhili wa muda mrefu wa Coastal Union, Nassor BinSlum amesema taarifa za kutekwa nyara kwa Mo Dewji zilimpa mshtuko wa hali ya juu na kuelekeza imani yake kwa vyombo vya dola vitafanikisha kumwokoa.

“Nimewaomba waumini wamwombee kwa Mungu huko aliko asidhurike, lakini niwasihi Watanzania waviache vyombo vya dola vifanye kazi yake,” alisema BinSlum.

Naye Mwenyeikiti Kamati ya Usajili ya Coastal Union, Hemed Hilal ‘Aurora’ aliitaka familia ya Dewji kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu huku wakiamini Mungu ndiye atakayetoa jibu la mtihani walioupata.

IMEANDIKWA NA KHATIMU NAHEKA NA MWANAHIBA RICHARD, DAR NA GODFREY KAHANGO, MBEYA, BERTHA ISMAIL, ARUSHA NA BURHAN YAKUBU, TANGA