Simba warejea kileleni

Muktasari:

Mabao ya Miraji Athuman dakika ya 39 na 74 huku Tairone Santos akifunga dakika ya 74 yalitosha kuipa ushindi Simba na kufunga mwaka kwa kishindo.
Huo ulikuwa mchezo wa mwisho kwa Simba kwenye ligi mwaka huu 2019, watarejea tena uwanjani Januari 4 mwakani watakapowakabili watani zao wa jadi Yanga kwenye Uwanja wa Taifa.

SIMBA imerejea kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifunga Ruvu Shooting mabao 3-0, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kutokana na matokeo hayo Simba imefikisha pointi 25 na kuishusha Kagera Sugar ambayo ilikaa kwa saa 24 kileleni baada ya jana Ijumaa kuifunga Lipuli mabao 2-1.
Mabao ya Miraji Athuman dakika ya 39 na 74 huku Tairone Santos akifunga dakika ya 74 yalitosha kuipa ushindi Simba na kufunga mwaka kwa kishindo.
Huo ulikuwa mchezo wa mwisho kwa Simba kwenye ligi mwaka huu 2019, watarejea tena uwanjani Januari 4 mwakani watakapowakabili watani zao wa jadi Yanga kwenye Uwanja wa Taifa.
Mpaka sasa Simba imecheza michezo 10, imeshinda minane dhidi ya JKT  Tanzania, Mtibwa Sugar, Azam, Kagera Sugar, Biashara United, Singida United, Mbeya City na Ruvu Shooting na imetoka sare mchezo mmoja dhidi ya Prisons huku ikipoteza mmoja dhidi ya Mwadui.
Katika  mchezo huo Simba ilicheza vizuri kuliko wapinzani wao jambo lililopelekea kupata ushindi huo.
Ushindi wa Simba ni kama maalum kumuaga kocha wao Patrick Aussems ambaye inadaiwa muda wowote anaweza kufungashiwa virago.
Licha ya viongozi kutosema sababu ya kutaka kumtimua kocha huyo Mbelgiji lakini mashabiki wengi wa Simba wanaonekana kutoafiki jambo hilo wakimtaka Aussems aendelee kufundisha timu yao.