Simba wapewa chao, Morrison awapa salamu

Muktasari:

Bao la dakika ya 79 la Benard Morrison jana dhidi ya Kagera Sugar liliipa pointi tatu muhimu Yanga, pia lilitosha kuwatikisa mashabiki wa Simba ambayo itakutana na Yanga Jumapili kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Dar es Salaam. Wape Salaam, ndivyo mashabiki wa Yanga wanavyowaambia Simba wakati huu homa ya pambano la watani wa Jadi ikiwa kubwa miongoni mwao huku mshambuliaji wao kipenzi Benard Morrison akiwa amerejea kikosini na kasi ya ajabu.

Bao la dakika ya 79 la Benard Morrison jana dhidi ya Kagera Sugar liliipa pointi tatu muhimu Yanga, pia lilitosha kuwatikisa mashabiki wa Simba ambayo itakutana na Yanga Jumapili kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Hivi karibuni Morrison aliingia matatizoni na uongozi wa klabu hiyo kuhusu mkataba wake wa usajili jambo lililoibua hasira kwa mashabiki wa klabu hiyo ambao walikuwa wakimtolea maneno makali kwenye mitandao ya kijamii kwa madai anawasaliti.

Hata hivyo, wakati mashabiki wakiamini mchezaji huyo hatacheza tena mpaka mwisho wa msimu, Kocha Luc Eymael alimrejesha kikosini na kupanga kumtumia katika mchezo wa jana dhidi ya Kagera Sugar na ule ujao wa FA dhidi ya Simba.

Licha ya Simba kukabidhiwa ubingwa hapana shaka hawakutaka kusikia Morrison amefunga katika mchezo wa jana kwani anawarudisha katika kumbukumbu ya mechi baina yao iliyofanyika Machi 8 mwaka huu, aliifungia Yanga bao pekee tena mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Katika mchezo huo, ulioanza kwa kasi huku timu hizo zikishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera, Yanga ilijipatia bao hilo dakika ya 79 baada ya Morrison kufunga bao tamu akimalizia pasi murua ya David Molinga.

Simba inakuwa mabingwa wa Ligi Kuu mara ya tatu mfululizo huku ikiwa imechukua mara 21 kihistoria tangu ligi ilipoanza mwaka 1965.

kwenye mchezo wao huo wa jana, timu zote zilicheza kwa kuviziana na kosakosa nyingi, huku dakika ya tisa tu Namungo ilikosa bao baada ya kiungo wake Lucas Kikoti kukiimbia na mpira na alipoingia ndani ya 18 alipiga shuti dogo lililopanguliwa na kipa Beno Kakolanya na kuuwahi akaudaka.

Simba nao walikosa bao dakika 14 baada ya shuti la Kagerekutoka nje kidogo ya lango.

Viungo wa Simba, Said ndemla, Mzamiru Yassin na Francis Kahata walionekana kutokuwa na mbinu za ziada katika kuwapenya viungo wa Namungo waliokuwa wanaongozwa na Lucas Kikoti.

Namungo ililazimika kumtoa Blaise Bigirimana baada ya kuumia kutokana na kugongana na kipa Beno Kakolanya na kuingia John Kelvin na hivyo safu yao ya ushambuliaji kudhoofika.

Kitendo cha Simba kumwanzisha Kagere kama mshambuliaji pekee kilionekana kuwanyima ushindi kwani mabeki wa Namungo hawakuwa na kazi nzito kumdhibiti.

Hata hivyo, katika mchezo huo licha ya mabadiliko yaliyofanywa na timu hizo, kwa Simba ya kuwaingiza Hassan Dilunga, Deo Kanda na Ibrahim Ajibu na kuwatoa Haruna Shamte na Francis Kahata na kuingia Cyprian Kipenye, huku Namungo aliingia Jamal Issa na kutoka Hashim Manyanya hazikusaidia kupata bao kwa pande zote.

Baada ya mchezo huo, waandaaji wa sherehe hizo waliwapa medali waamuzi waliochezesha mchezo huo, huku pia Namungo walienda kusalimiana na viongozi waliofika kushuhudia mchezo huo, wakiongozwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini, Wallace Karia na Waziri wa Utalii na Maliasili, Dk Hamis Kigwangala ambaye alikabidhi kombe hilo.

Sven, Kakolanya Waongea

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema “Ubingwa kwetu tulifurahia siku 10 zilizopita, tunashukuru tumemaliza ligi salama na ilikuwa safari ndefu,” alisema.

Kuhusu mechi ya nusu fainali dhidi ya Yanga alisema “Inabidi kwanza turudi Dar es Salaam baada ya hapo tutaweka mipango mengine,” alisema.

Kakolanya ambaye alidaka katika mchezo huo, alisema “Tunashukuru kumaliza mchezo salama licha ya kukutana na ugumu na hii imetokana na kila timu ilikuwa inahitaji matokeo,” alisema.

Katika mechi nyingine, Mbao ilishinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, Biashara na Ruvu Shooting zikitoka suluhu mjini Musoma, huku Ndanda wakitoka suluhu na JKT Tanzania mjini Mtwara.