Simba wamwagilia maji uwanja

Muktasari:

Try Again alisema walichukua uamuzi huo kwa vile wanatumia gharama kubwa kuwatunza wachezaji wao na mbali ya hilo wanajiandaa na michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika

SIMBA juzi Ijumaa waliamua kuingia gharama kumwagilia uwanja wa Mkwawani ili wachezaji wao wasiumie wakati wa mechi yao dhidi ya JKT Tanzania.
Uwanja huo wa Mkwakwani ni miongoni mwa viwanja vinavyotumika katika mechi za Ligi Kuu Bara na ligi zingine kuwa mbovu na mkavu jambo ambalo mara kwa mara huchangia kusababisha majeraha kwa wachezaji.
Kabla ya mechi hiyo iliyochezwa jana Jumamosi kocha wa Simba,  Patrick Aussems alilalamikia uwanja huo hivyo viongozi wa simba waliona kuna haja ya wao kumwagilia maji angalau kupunguza makali ya ubovu wa eneo la kuchezea.
Try Again alisema walichukua uamuzi huo kwa vile wanatumia gharama kubwa kuwatunza wachezaji wao na mbali ya hilo wanajiandaa na michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika
"Huo uwanja ni mbaya sana. Sipo Tanga lakini nimeambiwa hali halisi ya huko ndio maana nikaagiza angalau umwagiliwe maji kwa gharama zetu.
"Tumetumia gharama kubwa lakini ni bora kujikinga mapema kuliko kuacha wachezaji waumie. Tungepata hasara kubwa kwa kuanza kuwauguza wachezaji pengine kuuguza kwa muda mrefu na kuwakosa kwenye michuano mikubwa," alisema Try Again.
Meneja wa uwanja huo Nassoro Makau alikiri Simba kumwagilia uwanja huo jana baada ya kuomba wafanye hivyo kunusuru afya za wachezaji wao.