Simba walala kitajiri Eswatini

Muktasari:

  • Simba inatarajiwa kurudiana na Mbabane Swallows kesho katika mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo kama itasonga mbele itapata nafasi ya kucheza ama na Nkana ya Zambia au UD Songo ya Msumbiji.

Mbabane, Eswatini.Msafara wa Simba umetua salama nchini Eswatini (Swaziland) usiku wa jana imeonyesha jeuri ya fedha kwa kulala katika hoteli ya kifahari nchini humo.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, wamefikia kwenye hoteli ya kifahari ya Royal Swazi SPA ambayo gharama ya chumba kimoja ni kiasi cha Dola 399 (zaidi ya Sh790, 000) kwa usiku mmoja.

Hoteli hiyo iliyopo umbali wa kilomita 6 kutoka uwanja wa Somhololo ambao utachezwa mechi yao dhidi ya Mbabane Swallows una huduma za hadhi ya juu zinazoifanya iwe moja ya hoteli maarufu nchini humo.

Kiujumla hoteli hiyo ina vyumba 149 vya kulala, kumbi kubwa za mikutano, baa kubwa mbili, casino, uwanja wa kuchezea gofu, mabwawa ya kuogelea na kadhalika.

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi ameiambia Mwanaspoti kuwa mazingira ya hoteli hiyo ni tulivu na yenye usalama.

“Tumefika salama hapa Eswatini (Swaziland) na tumefikia katika hoteli ya Royal Swazi SPA. Kila kitu kipo sawa na maandalizi yanaenda vizuri," alisema Nghambi.