Simba waita mashabiki washuhudie watakachowafanya Azam FC

Muktasari:

Simba ndio bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara. Endapo wataibuka na ubingwa msimu huu wa 2018-2019, utakuwa wa 20 kwao na watashika nafasi ya pili baada ya vinara Yanga wanaoongoza kwa kuchukua mara 27.

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Klabu ya
Simba, imewaambia mashabiki wake wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Uhuru leo Jumatatu jioni kwa wingi kwa ajili ya kukishangilia
kikosi hicho kitakapokuwa kinachuana na Azam FC.
Simba ambao ni vinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 81, Yanga ikishika nafasi ya pili na pointi 80 wakati Azam FC wakishika nafasi ya tatu na pointi 68.
Inakutana na Azam FC katika mechi ya marudiano ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa saa 10:00 jioni baada ya ule wa kwanza kumaliza na ushindi wa mabao 3-1.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema, kikosi chake kipo
tayari kwa mchezo huo na wana imani ya kuibuka na ushindi.
"Timu iko vizuri kilichobaki ni kutimiza wajibu wetu uwanjani.
Azam FC ni timu nzuri kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa
kujituma anavyoweza,"alisema Aussems.