VIDEO: Simba wafunga mitaa Dar

Muktasari:

Kikosi cha Simba kiliwasili saa 4:37 na moja kwa moja wachezaji waliingia katika gari aina ya Coastal kisha walishuka na kupanda gari ya wazi aina ya Canter.

MASHABIKI wa Simba wamejitokeza kwa wingi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere 2 kwa ajili ya kuipokea timu hiyo iliyotwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Simba walicheza fainali hizo jana Jumapili Agosti 2, 2020 dhidi ya Namungo, mechi iliyochezwa Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga ambapo Simba walishinda bao 2-1.

Simba wamewasili uwanjani hapo saa 4:37 na moja kwa moja wachezaji waliingia katika gari aina ya Coaster kisha walishuka na kupanda gari ya wazi aina ya Canter.

Baada ya kupanda katika gari hilo, msafara wa kutoka uwanjani ulianza huku mashabiki wakiukimbiza kwa miguu mpaka walipofika barabara kubwa.

Mashabiki hao waliokuwa wanaendesha bodaboda hawakuwa nyuma kwani waliufuata msafara huo kwa mbwembwe barabarani huku kila mmoja akionyesha  utundu wa kutumia chombo hicho cha moto.

Mashabiki hao hawakuwa na hiyana kwani walikuwa wanaenda hatua kwa hatua mpaka msafara ulipofika Makao Makuu ya Simba msafara huku mashabiki wao wakiwa wanawashangiia muda wote.

Polisi walihakikisha msafara huo hauingiliwi na mtu asiyehusika kwani walikuwa wanahakikisha usalama unakuwepo wa kutosha.

 

MWENDOKASI YAFUNGWA

Kutokana na tukio hili usafiri wa mwendokasi ulifungwa kwa muda kutokana na gari za msafara wa Simba kusimama katika barabara hizo.

Ufinyu wa eneo ulilazimu kuwa na msongamano katika eneo hilo hata pale ambapo polisi walijitahidi kufungua njia bado mwendokasi zilikuwa zinapita kwa tabu kwa sababu watu walikuwa wamesimama mpaka barabara hizo.

Hili ni taji la tatu msimu huu kwa Simba ambapo wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Ngao ya Hisani.