Simba vs AS Vita : Simba inapenya hapa

Muktasari:

  • Hivi ndio jinsi kikosi cha Kocha Mbelgiji Patrick Aussems kitakavyoweza kupambana na kupata upenyo.

SIMBA imebakisha nafasi moja tu ya kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kama ikichemsha kwenye mchezo huo wa mwisho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya AS Vita, safari yao itakuwa imeishia hapo.

Itakuwa ni vita kali, kwani hata Vita nao wanaisaka nafasi hiyo na kama wakishinda tu wanasonga hatua inayofuata.

Benchi la ufundi na viongozi watafanya yao, lakini kazi kubwa itakuwa kwa wachezaji ambao wataingia uwanjani. Hili bato si la mchezo buana, atakayezubaa ameliwa.

Hivi ndio jinsi kikosi cha Kocha Mbelgiji Patrick Aussems kitakavyoweza kupambana na kupata upenyo.

Manula - Lukong

Ushindani wa kwanza utakuwa katika eneo la makipa na kwa upande wa Simba, atasimama langoni Aishi Manula. Anakazi kubwa ya kuwapanga wachezaji wake ili kuondoka na ushindi. Katika mechi tatu za karibuni za michuano hiyo ya Afrika Manula ameruhusu mabao 12 rekodi ambayo sio ya kujivunia lakini ana nafasi ya kubadilika.

AS Vita wao wataanza na kipa wao mzoefu, Nelson Lukong ambaye pia hatakuwa na kazi rahisi katika mchezo huo hasa baada ya uwepo wa mastraika wa Simba John Bocco, Meddie Kagere na kurejea kwa Emmanuel Okwi ambaye hakwenda Algeria kumenyana na JS Saoura.

Okwi - Bangala

Kuna dalili katika winga ya kushoto ataanza Okwi. Hata hivyo, haitakuwa kazi rahisi kuipenya ngome ya ulinzi ya AS Vita kwani atakuwa akikabwa na beki wa kulia, Yannick Bangala.

Katika mechi ya kwanza Kinshasa Kongo Simba wakikubali kichapo cha mabao 5-0, Okwi alionekana kuzidiwa na Bangala ambaye muda mwingi alionekana kupanda katika kuanzisha mashambulizi na kukaba.

Okwi atatakiwa kutumia akili nyingi sana kuweza kumpita beki huyo ili kuisaidia timu yakekutinga robo fainali.

Chama - Muzinga

Kiungo wa Simba, Cletus Chama amekuwa kama chumvi kwa timu yake msimu huu, amekuwa kichocheo cha mabao, kama atakuwa katika ubora wake, atafanya vizuri. Hata hivyo, katika mechi za karibuni kiwango kimekuwa kikusuasua.

Chama katika mchezo huo huenda akaanza kama winga wa kulia ambaye muda mwingi hucheza katikati ya uwanja.

Si mzuri sana katika kukaba lakini ni mahiri katika kuanzisha mashambulizi na kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji ingawa muda mwingine hufunga mwenyewe.

Katika mechi hii Chama atakutana na kibarua cha kumzidi ujanja beki wa kushoto wa AS Vita, Ngonda Muzinga ambaye naye ni mahiri katika kuzuia mashambulizi hasa kutoka kwa wachezaji wabunifu kama Chama.

Bocco - Makwekwe

Nahodha wa Simba, John Bocco ni muhimili mkubwa hasa eneo la ushambuliaji. Muda mwingi amekuwa akiwasumbua mabeki wa timu pinzani.

Bocco ameonekana kuimarika zaidi katika kufunga na hata muda mwingine hutengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji wenzake na katika mchezo huu atakuwa chini ya ulinzi wa beki mwenye uwezo wa kuruka vichwa, Makwekwe Kupa ambaye alifunga bao la tatu katika mechi ya kwanza walipokutana kwenye mchezo wa kwanza.

Kagere - Bompunga

Kinara wa mabao katika kikosi cha Simba msimu huu Meddie Kagere amekuwa mwiba kwa walinzi wa timu pinzani kwani muda wowote wakifanya makosa amekuwa akiwaadhibu kwa kufunga bao hata mazingira ambayo hayakutegemewa.

Botuli Bompunga ni mrefu mwenye nguvu kama Kagere ambaye amekuwa akicheza kwa muda mrefu kwenye kikosi cha kwanza cha AS Vita akielewana sana na Makwekwe watakuwa na kazi ya kuwazuia Kagere na Bocco.

Kagere mbali na kuwa na uwezo wa kufunga, lakini amekuwa na maelewano makubwa na Bocco, muda mwingine wamekuwa wakitengenezeana nafasi za kufunga na wameweza kufanya hivyo katika mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mzamiru - Nelson Munganga

Katika mechi na AS Vita Simba watamkosa kiungo wa Jonas Mkude ambaye anatumikia kadi, nafasi yake huenda ikatua kwa Mzamiru Yassin ambaye muda mwingine amekuwa akicheza katika eneo hilo la kiungo.

Mzamiru ni mzuri katika kukaba na kushambulia na kwa mara ya kwanza anaweza kuanza katika kikosi cha kwanza cha Simba lakini atakutana na changamoto ya kumpita au kumzidi maarifa kiungo mkabaji wa AS Vita Nelson Munganga.

AS Vita ni wazuri katika eneo la kiungo sawa na Simba, mabao mengi yamekuwa yakianza kusukwa katika eneo hilo kwa maana hiyo kati ya Mzamiru na Munganga, atakayekuwa bora ndio timu itamaliza vizuri dakika tisini.

Tshabalala - Kisinda

Beki wa kushoto, ambaye anapewa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha Simba Mohammed Hessein ‘Tshabalala’ atakuwa na kibarua cha kumzuia winga wa AS Vita Tuisila Kisinda.

Katika mechi ya kwanza Kisinda alionekana kumsumbua sana Asante Kwasi, ambaye alianza katika kikosi cha kwanza kwa maana hiyo Tshabalala katika mechi hii hatakuwa na kazi nyepesi.

Kotei - Ngoma

Kiungo mkabaji wa Simba Mghana James Kotei amekuwa roho na nguzo imara katika kikosi hicho.

Katika mechi ya kwanza hakuwa bora sana, alipotezwa na viungo wa AS Vita hasa Luamba Ngoma ambaye ndio roho ya kutengeneza mabao katika kikosi hicho.

Ngoma ni mzuri katika kupiga pasi za mwisho na amekuwa akihusika katika mashambulizi muhimu ya AS Vita kwa maana hiyo haitakuwa kazi rahisi kwa Kotei.

Juuko - Makusu

Juuko Murshid alikosekana katika mechi iliyopita dhidi ya JSS kwa kuwa alikuwa anatumikia kadi mbili za njano lakini kutokana na mapungufu ambayo yapo katika kikosi cha Simba anapewa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza.

Katika mechi ya kwanza straika wa AS Vita Jean-Marc Makusu aliweza kufunga mabao mawili katika ushindi 5-0, lakini aliwasumbua safu ya ulinzi ya Simba ambayo ililazimika kufanya makosa mengi hasa mipira ya krosi.

Katika mchezo wa Jumamosi, Juuko na Makusu ambaye atakuwa bora katika kutimiza majukumu yake ndio ataweza kuifanya timu yake kutimiza lengo la kuondoka na ushindi ili kusonga mbele.

Wawa - Kasengu

Beki wa kati mzoefu wa Simba Pascal Wawa ndio mchezaji aliyecheza mechi nyingi katika kikosi hicho katika mashindano yote msimu huu, kwenye mchezo dhidi AS Vita atakutana na kibarua cha kumkaba Kazadi Kasengu.

Kasengu, ambaye muda mwingine anacheza akitokea pembeni naye amekuwa na maelewano na Makusu katika kuwasumbua safu ya ulinzi wa timu pinzani na ili asiwe mwiba kwa Simba Wawa anatakiwa kumchunga mwanzo mwisho.

Coulibaly - Tonombe

Mlinzi wa kulia katika kikosi cha Simba ataanza Zana Coulibaly, ambaye amekuwa na kiwango kinachoimarika tangu alivyocheza vizuri mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ambayo walishinda bao 1-0.

Katika mechi na AS Vita atakuwa na kazi ya kumzuia winga Mukoko Tonombe, ambaye muda mwingine huonekana kucheza ndani kama mshambuliaji wa kati.

Tonombe anaweza kupiga krosi zenye macho kwa washambuliaji, pia mzuri katika kupiga chenga na kuingia katika eneo la hatari la timu pinzani, kwa maana hiyo kati yake na Zana, ambaye atakuwa imara ndio ataisaidia timu yake kufanya vizuri.