Simba nusura imtoe machozi baba wa Samatta

Muktasari:

  • Asikuambie mtu mashabiki hasa wa Simba na Yanga wanaumia sana pale wanapokumbana na matokeo ambayo hawakuyatarajia na ndicho kilichotaka kumtokea baba yake na Mbwana Samatta

BABA mzazi wa mwanasoka wa kimataifa, Mbwana Samatta anayejulikana kwa Ally Pazi Samatta ametoa kali ya mwaka baada ya kutamka kuwa Simba imemtoa aibu kuifunga As Vita ya Kongo na kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Anasema alikuwa anasijikia kuangua kilio mpaka pale aliposikia Simba wamefunga bao la pili kupitia kwa  Mzambia Claytous Chama ndipo akajisikia homa imekata ghafra mwilini.

"Mechi ilivyokuwa inaendelea nilikuwa najisikia homa mwili mzima, kutetemeka sio kutetemeka, machozi yalikuwa yananilengalenga kiasi kwamba dakika 90 zingemalizwa kwa sare nadhani ningeumbuka.

"Maana ningeangua kilio ambacho nisingekuwa na maelezo nacho, kiukweli Simba imenifanya niwe mwenye furaha, hatua ya robo fainali wachezaji wanapaswa kuongeza umakini zaidi kuhakikisha wanafika fainali za ligi ya Mabingwa Afrika,"anasema.

Mwenyekiti wa zamani wa timu hiyo, Hassan Dalali 'Mzee Dalali' naye hakuwa nyuma kutoa maoni yake kwamba kutinga hatua ya robo fainali si kitu kidogo na kushauri cha kufanya wachezaji kwamba ni kujiamini.

"Wamefanya kazi kubwa, akili zao ziamini kwamba wanaweza wakaandika historia ya kuchukua ubingwa wa Afrika, timu wanazokutana nazo kwenye hatua hiyo sio ngeni kwao,"anasema.