Simba moto uleule

TAIFA Stars inakipiga leo kwenye Uwanja wa Mkapa na Burundi, lakini Simba hawataki masihara kabisa. Wanaendelea na ratiba ya tizi jijini Dar es Salaam kujiweka sawa na mechi za Ligi Kuu Bara.

Simba itakipiga na Tanzania Prisons kwenye mechi ya ligi Oktoba 22. Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu wametoa wachezaji sita Stars huku wengine wanne wakiitwa katika mataifa yao.

Simba katika kuhakikisha kwamba inakwenda na moto uleule haijapoa baada ya kupata mapumziko yaliyotokana na kalenda ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa), ni kama wameongeza dozi kwani kocha wao Sven Vandenbroeck ameamua kwamba sasa ni matizi kwa kwenda mbele.

Wachezaji wanaoendelea na ratiba ya Sven ni wale wote ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa wakiwemo mastaa wawili Clatous Chama na Luis Jose ambao hawakwenda kuchezea timu za mataifa yao kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa juzi na jana walikuwa na programu mbili kali asubuhi na jioni ambapo wanadamkia gym halafu jioni wanakwenda uwanjani kuuchezea mpira na kujazwa mambinu.

Kwa mujibu wa Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu Sven hajaweka rasmi ratiba, lakini kila siku hutoa mpangilio mpya na wa kisasa kuhakikisha wachezaji hao hawatoki kwenye mstari na wanakuwa fiti kama kawaida, lakini mara mbili ni lazima.

Kocha wa viungo, Adel Zrane ndiye amekuwa akiwapigisha gym ya maana mastaa wa timu hiyo asubuhi na ameposti kwenye ukurasa wake kwamba sasa ni mwendo wa tizi tu.

Simba inawakosa nyota Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, John Bocco, Jonas Mkude na Said Ndemla ambao wapo na Taifa Stars.

Wengine ni Meddie Kagere aliyeitwa Rwanda, Joash Onyango na Francis Kahata wao wameitwa nchini kwao Kenya.

Sven ana malengo ya kutetea ubingwa huo tena, ikiwa hivi sasa wanashika nafasi ya pili katika msimamo wakiwa wamekusanya pointi 13 na kucheza mechi tano ambapo wapo nyuma ya Azam FC wanaoongoza ligi kwa pointi 15.

Rweyemamu aliliambia Mwanaspoti kuwa kocha wao harembi kwani kila kitu kinakwenda kama anavyopanga ili ligi itakapoendelea wachezaji wawe na utimamu wa mwili na watimize malengo yao kwa uharaka zaidi.

“Haweki wazi mipango yake ila akihitaji leo yafanyike mazoezi ya aina fulani, basi hufanyika, ndiyo maana tunaenda gym na uwanjani,” alisema Rweyemamu na kusisitiza kwamba kila kitu kinakwenda vizuri na amefurahia morali na mzuka wa wachezaji.

Simba itacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Ndanda Jumanne na Jumamosi na Mlandege.